Anayedaiwa kuchoma moto nyumba na watu wanne kuteketea Handeni akamatwa

Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga  limemkamata Mwita Chacha akiwa jijini Mwanza kwa tuhuma za kuchoma nyumba moto katika Kijiji cha Manga, Wilaya ya Handeni Desemba 30, 2024 na kusababisha mauaji.

Waliofariki dunia katika tukio hilo ni Pili Saguge (28) mkazi wa Kwedichocho na watoto wake Chacha Nyabilenga, Jane Nyabilenga na Makabala Nyabilenga.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumanne  Januari 7, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi  amesema tukio hilo lilisababisha vifo vya watu wanne, wakiwamo mama na watoto wake watatu.

Amesema mtuhumiwa anadaiwa kutekeleza mauaji hayo ya kikatili kutokana na madai kuwa, familia ya marehemu Pili Saguge, ilimpa sumu mtoto wake.

Kamanda Mchunguzi amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa amejificha jijini Mwanza na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yake.

Amesema miili ya watu hao wanne ilikutwa ikiwa imeungua kwa kiwango kikubwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa mtuhumiwa Mwita Chacha kwa tuhuma za kuchoma nyumba moto Tanga. Picha na Rajabu Athumani

Akielezea tukio hilo, Paul Daniel ambaye ni mume wa marehemu, amesema kabla ya tukio hilo, alisafari kwenda  Dar es Salaam kwa shughuli zake za utafutaji na aliporudi, alikuta familia yake ya watu wanne wameuawa kwa kuchomwa moto.

Amesema, mtuhumiwa anayedaiwa kufanya tukio hilo, hakuwahi kuwa na ugomvi na yeye isipokuwa kuna siku alimuita nyumbani kwake wamzike mtoto wake, lakini Paul alikataa kwa kusema anaenda kuita watu wengine ndio waendelee na maziko.

Wakati huohuo, Kamanda amesema jana Jumatatu  Januari  6, 2025, saa 8:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga lilifanikiwa kumkamata  Hamisi Hamisi (21), mkazi wa Majani Mapana kwa tuhuma za kuiba vitu mbalimbali katika nyumba moja ya mwananchi huko Uzunguni Kange.

“Mtuhumiwa amekutwa na bastola  aina ya Kevin-ZVI yenye  namba H06403, magazine mbili za bastola bila risasi, laptop mbili, saa sita za mkononi, sime moja, nyundo, nondo, miwani, funguo mbili,boksi la simu, shanga ya kiunoni na sabuni tatu za kuogea ambavyo ni miongoni vya vitu vilivyoibwa siku hiyo ya tukio,”amesema Kamanda Mchunguzi.

Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu kupitia njia rasmi za mawasiliano.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawahimiza baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kuficha wahalifu au kuwapa hifadhi, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Related Posts