Mzee adaiwa kujinyonga kisa msongo wa mawazo

Shinyanga. Joseph Tuju (73) mkazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Lubaga, Halmashauri Manispaa ya Shinyanga amefariki dunia kwa madai ya kujinyonga kwa kutumia shuka akiwa ndani ya nyumba yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema, “taarifa hizi nimepokea Januari 6, 2025 saa 12 jioni na kwa uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi chanzo cha mtu huyo kujinyonga ni msongo wa mawazo kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu, ingawa hayajulikani na mwili umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya shughuli za mazishi.”

Katika tukio hilo,  Januari 06, 2025 jioni majirani walipoona nzi wengi wakizunguka nyumba ya mzee huyo, waliamua kuvunja mlango na kuingia ndani na kukuta mwili wa Tuju ukining’inia.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 7, 2025, baba mdogo wa marehemu John Kisandu amesema kuwa, alipopata taarifa za  mtoto wake kujinyonga,  alipokwenda nyumbani kwake na  alikuta nzi wamejaa kuzunguka nyumba hasa kwenye madirisha na mlango.

“Huyu ni mtu wa nne kujinyonga katika familia yetu, alianza mama yake mzazi aliyejinyonga, akafuata mdogo wake akajinyonga, dada yake akajinyonga na sasa hivi kafuata yeye kajinyonga, na kuna mdogo wake alijaribu kujinyonga lakini alinusurika,” amesema Kisandu.

Jirani wa familia hiyo ya marehemu, Masele Sagenge ameeleza namna walivyogundua tukio hilo akisema alikuwa anapalilia, jinsi alivyokuwa anasogea akaona kama nzi kwenye nyumba ya jirani.

“Nilikuwa napalilia, jinsi nilivyokuwa nasogea nikaona kama nyuki kwenye nyumba ya mzee Tuju,  baadaye nikasikia harufu, halafu kuna nzi nilivyosogea nikaona nzi wengi ndio nikamwita jirani mwingine,” amesema Sagenge.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Azimio, Masanja Liso ameeleza hali ya matukio ya watu kujinyonga katika mtaa huo, akisema katika familia ya mzee Tuju imekuwa kama mtu akijisikia kujiua anafanya tukio hilo.

“Taarifa hii nimepokea saa 10 jioni, ndipo nilipokuja na kukuta hali ilivyo, nikapiga simu polisi na kusubiri maelekezo yao,” amesema Liso.

Diwani wa Lubaga, Reuben Dotto ametoa rai kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi pindi wanapokumbana na changamoto kwenye maisha  akisema ni vyema kushirikisha watu ili kupata ufumbuzi.

“Ni jambo la kushangaza kwa Mungu na sheria, na ndio maana mtu akinusurika anachukuliwa hatua za kisheria na kama kuna mtu ana changamoto ashirikishe watu ili kupata ufafanuzi sio kuchukua uamuzi haraka,” amesema Dotto.

Related Posts