KITENDO cha kufungwa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso, kimeonekana kumkera Kocha wa Zanzibar Heroes, Ali Bakar Ngazija.
Zanzibar Heroes imepokea kipigo hicho juzi katika mchezo wao wa pili wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 inayofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Katika mchezo huo, bao la Burkina Faso lilifungwa na mshambuliaji Abubar Toure dakika ya 74.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Ngazija alisema kipigo hicho kilitokana na safu yake ya ushambuliaji kukosa umakini jambo lililowafanya wapinzani wao kuondoka uwanjani wakiwa wababe.
Alisema wachezaji wake walipata nafasi nyingi za kufunga lakini umakini mdogo waliokuwa nao umewagharimu na kukosa alama tatu ambazo endapo wangezipata zingewaweka nafasi nzuri ya kucheza fainali.
“Tumekubali tumefungwa lakini tulipata nafasi nyingi wachezaji wangu wameshindwa kuzitumia,” alisema kocha huyo na kuongeza.
“Nimeona mapungufu kwenye maeneo ya ushambuliaji hibyo tutakwenda kuyarekebisha tupate ushindi mchezo unaofuata ili tufuzu fainali.”
Hata hivyo, kocha huyo aliwataka mashabiki na wapenzi wa Zanzibar Heroes kutokana tamaa na kuendelea kutoa sapoti hadi mwisho ili kubeba ubingwa wa michuano hiyo.
Zanzibar Heroes ilianza michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya ndugu zao Kilimanjaro Stars, huku ikibakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Kenya utakaochezwa Januari 10.
Kipigo hicho kimeifanya Zanzibar Heroes kubaki na pointi tatu huku Burkina Faso ikifikisha nne. Wakati Kenya (1) na Kilimanjaro Stars (0) zikicheza jana usiku.
Leo Jumatano ni mapumziko kisha michuano hiyo itaendelea kesho Alhamisi kwa Kilimanjaro Stars kukabiliana na Burkina Faso, huku Ijumaa ni Zanzibar Heroes dhidi ya Kenya. Timu mbili zitakazokuwa na pointi nyingi baada ya hapo, zitacheza fainali Januari 13.