Kagera Sugar yafuata mido Kenya

KLABU ya Kagera Sugar, imefikia makubaliano ya awali na kiungo wa Tusker FC, Saphan Siwa Oyugi, kwa ajili ya kumsajili kama mchezaji huru.

Hata hivyo, ingawa taarifa za awali zimesambaa kwamba usajili huu umekamilika, bado haijathibitishwa rasmi na klabu ya Kagera Sugar au Tusker FC.

Kwa mujibu wa vyanzo, pande zote mbili zimefikia makubaliano ya kimsingi na Saphan anatarajiwa kuwasili Tanzania katika siku chache zijazo ili kumalizia taratibu za mwisho za mkataba.

Iwapo makubaliano hayo yatathibitishwa, Saphan atajiunga na Kagera Sugar kwa ajili ya kuimarisha safu ya kiungo ya timu hiyo.

Akizungumzia maboresho yanayoendelea katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, kocha wa Kagera Sugar, Melis Medo alisema: “Tumeamua kufanya maboresho ya nguvu kwa sababu tunataka kuwa bora zaidi katika awamu iliyosalia ya ligi, naamini tunaweza kufanya vizuri na kusogea nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.”

Kagera Sugar ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11 katika michezo 15 iliyocheza hivyo ina kazi kubwa ya kufanya katika duru la pili la ligi hiyo kuhakikisha inajiondoa katika hatari ya kushuka daraja.

Related Posts