Wako wapi wanafunzi 538,526 waliotakiwa kufanya mtihani kidato cha sita?

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mpango wake wa elimu bila malipo, wadau wa elimu wanasema mzigo wa mahitaji binafsi ya mwanafunzi ni miongoni mwa changamoto inayowadondosha wanafunzi katika mfumo rasmi wa elimu.

Takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaonyesha wanafunzi 538,526 miongoni mwa 652,031 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2018 wameshindwa kufika kidato cha sita.

Hii inamaanisha ni mwanafunzi mmoja pekee kati ya sita ndio amefika kidato cha sita na kutahiniwa. Wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka 2018, mwaka huu wanapaswa kumaliza kidato cha sita.

Takwimu hizo zinaungwa mkono na taarifa iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Jumapili ya Mei 5, 2024 kuwa wanafunzi 113,504 wanatarajia kufanya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu. Mtihani huo ulianza Mei 6 na utamalizika Mei 24 mwaka huu.

Kwa kawaida wapo wanafunzi wanaoanguka katika ngazi mbalimbali za elimu, ila anguko kubwa lilitokea wakiwa kidato cha nne ambapo ni mwanafunzi mmoja pekee kati ya wanne ndio aliendelea kidato cha tano.

Mwaka 2021 walioandikishwa kidato cha nne walikuwa 485,884 na mwaka 2022/2023 walioandikishwa kidato cha tano walipungua hadi kufikia 102,722. 

Akitoa mtazamo wake kuhusu idadi ya wanafunzi waliotoka nje ya mfumo rasmi wa elimu, mhadhiri mstaafu Dk Godfrey Malisa anasema shida ipo kwenye gharama ya kusoma akizungumzia mahitaji binafsi ya mwanafunzi.

“Mwanafunzi anapofika kidato cha kwanza ndipo anapoanzia utu uzima hadi anapofika kidato cha nne amekuwa mtu mzima tayari. Anakuwa mzigo kwa familia yake, hivyo haoni faida ya kuendelea kusoma kwa hiyo anaingia kidato cha tano na sita ili afanye nini? ”anahoji daktari huyo.

Dk Malisa anasema kwa mataifa ya nje elimu ya kidato cha tano na sita, ilishafutwa kutokana na kutokuwa na faida yoyote na badala yake kugeuzwa kuwa elimu ya chuo.

Hii ni tofauti na Tanzania aliyoitolea mfano kuwa, mtu anapomaliza kidato cha nne, atapaswa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita ambayo hayana mchango wowote kwake.

Dk Malisa anaijenga hoja yake kwamba, kutokana na wanafunzi kutoona umuhimu wa kujiunga na ngazi hiyo ya elimu hulipiga teke daraja hilo, ugumu wa maisha ukiwa na mchango mkubwa.

“Mabadiliko yoyote yatakayofanyika kwenye sekta ya elimu yaendane na mahitaji ya wanafunzi, hatuwezi kuwa na kidato cha tano na sita ambavyo havina faida zozote, hata hao wanaomaliza kidato cha sita na hatimaye vyuo,  wanahangaika na kuambiwa wajiajiri, sasa kwa nini mtu asimalize darasa la saba akajifunza ufundi akajiajiri?”ameeleza.

Badala ya kuendelea kuwa na kidato cha tano na sita, Dk Malisa amesema ni muhimu kuweka mkazo wa mafunzo kwa vitendo ili kuwapa ujuzi wanafunzi wanaohitimu vyuo.

Jambo la pili analolinyooshea kidole ni suala la walimu,  ambalo anasema wengi  uwezo wao ni mdogo katika kutoa ujuzi kwa wanafunzi.

Hoja hizo hazitofautiani na za  mdau wa elimu, Ziada Mgalla,  anayesema suala la elimu nchini watoto wengi hawapati matokeo waliyotaraji wakiwa shuleni,  hivyo wanapofika kidato cha nne hudondoka.

“Hata ukiangalia matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana wanafunzi wengi hawakufuzu kwenda kidato cha tano, kwa hiyo wanafunzi wengi tunawapoteza kidato cha nne kutokana na kutofanya vizuri,” amesema.

Hoja nyingine anayoibua ni uchache wa madarasa ambayo inachangia hata baadhi ya wanafunzi waliopata daraja la tatu, kushindwa kupata nafasi ya kuendelea na masomo.

Anadokeza  suala la ufundishaji akisema fani ya ualimu imekuwa ajira,  hivyo hata walimu uwezo wao wa kufundisha si mkubwa. 

Kutokuwepo kwa motisha, sifa za ufundishaji kuwa chini, mishahara midogo, kukosa furaha na taaluma ya ualimu vinakwaza uendelevu wa sekta hiyo amesisitiza Ziada.

“Ni kiasi gani Serikali inawekeza kwenye elimu kuhakikisha walimu wanawezeshwa kuwa na zana za kufundishia ili wanafunzi wafaulu? Jambo lingine ni lugha limekuwa tatizo wanafunzi wanamaliza darasa la saba hawawezi kusoma kwa Kiingereza kwahiyo anapokuwa anafundishwa kwa lugha ambayo haielewi wengine wanaacha shule,” amesema.

Hoja hizo zinaibua mtazamo mwingine kwa mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko anayesema idadi hiyo ya wanafunzi wasioonekana ni wanafunzi walioshindwa shule na kuishia mitaani,  huku baadhi ya walioshindwa kufika kidato cha tano wakiwa  wale waliochagua kujiunga na vyuo baada ya kumaliza kidato cha nne.

Akichambua mtazamo wake, anasema suala la watu kutoona umuhimu wa kuendelea kidato cha tano unatokana wakati mwingine na kushuka kwa thamani ya elimu kutokana na waliomaliza vyuo kubaki mtaani.

“Kuna watu wanaona hakuna haja ya kuendelea kidato cha sita hadi chuo kwa sababu hata akiishia kidato cha nne, anaweza kupata maisha sawa na hao waliosoma, hivyo wanaamua kutafuta fursa za ajira mapema,”amesema.

Amesema kushindwa kuendelea kwa wanafunzi wakati mwingine kunatokana na kufeli mitihani hususani ya kidato cha pili na nne.

Licha ya kuwa mtihani wa kidato cha pili unatoa nafasi ya mtu kuendelea na darasa ikiwa atafeli mara mbili,  lakini   Nkoronko amesisitiza tafiti zinaonyesha kuwa wengi hukata tamaa ya kuendelea na shule.

“Wakati mwingine pia ni mfumo wa kijamii inafanya wanafunzi wengi kuacha shule hasa mwamko wa wazazi katika elimu unapokuwa mdogo,” amesema Nkoronko. 

Related Posts