Dar es Salaam. Wabunifu wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, wametakiwa kuboresha ujuzi na maarifa ili kukuza soko la vifaa hivyo na kuhimili athari za mabadiliko tabianchi.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Januari 7, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufundi Juu ya Upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia, Ngereja Mgejwa katika mafunzo ya siku tatu kwa wabunifu wa teknolojia ya nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema ujuzi kwa wabunifu wa teknolojia hizo utasaidia kukuza soko la vifaa na kuhimili mabadiliko tabianchi.
Mafunzo hayo, yameandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa na Uwekezaji (UNCDF) kupitia programu ya nishati safi ya kupikia, inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), Wizara ya Nishati na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
“Programu hii, ni sehemu ya mpango mkubwa wa CookFund wa miaka mitano (2021-2026), unaolenga kuchangia mafanikio ya Tanzania na kuongeza idadi ya watu wanaotumia nishati safi ili kutunzaa mazingira,” amesema Mgejwa.
Amesema washiriki waliopangwa kuhudhuria mafunzo hayo, ni wale walioteuliwa na wanaojishughulisha na maendeleo ya teknolojia zinazotumika kwenye nishati safi.
“Mkakati wa kitaifa, unalenga hatua muhimu ambazo zinasaidia lengo la kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema Mgejwa.
Hatua hizo, amesema ni kuongeza upatikanaji wa malighafi za uzalishaji, kukuza uwekezaji katika sekta ya kupikia, kupanua upeo wa utafiti na ubunifu na kujenga uwezo wa watendaji.
Meneja wa Programu ya CookFund, Imanuel Muro amewahimiza washiriki kuunda ushirikiano utakaosaidia kueneza mawazo yao.
“Sekta ya nishati safi, inatambuliwa kama sekta muhimu katika kufikia malengo ya Tanzania ya mabadiliko ya tabianchi na nishati, hatua hii, inatoa fursa kubwa ya kibiashara kwa wabunifu wenye suluhisho linalohusiana na mkakati huu, hapa nchini,” amesema Muro.
Sambamba na hilo, amesema mpango wa CookFund unalenga kusaidia wajasiriamali na biashara ili kushughulikia vikwazo, vinavyohusiana na upatikanaji wa bei nafuu ya vifaa vinavyotumika.