Morogoro. Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imepanga kujenga kituo cha pamoja cha wafanyabiashara wa vyakula na mbogamboga, ambao kwa sasa wanaendesha shughuli zao kando mwa barabara za katikati ya mji, ikiwamo ya Boma na ya zamani ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Manispaa ya Morogoro (DCC) kilichowakutanisha wakuu wa idara za halmashauri, viongozi wa dini, siasa, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo amesema usanifu wa ujenzi wa kituo hicho katika eneo la Mlapakolo tayari umekamilika.
“Changamoto hii bado ni kubwa, na tunaendelea kulifanyia kazi. Kwa sasa tunafikiria kujenga masoko mengine mapya,” amesema Mkongo.
Amesema biashara za barabarani zinazorotesha juhudi za usafi wa mji na kusababisha usumbufu kwa watembea kwa miguu na wenye vyombo vya moto.
“Aidha, kuna watu wanauza vyakula nje ya maduka nyakati za usiku, hali inayoweza kusababisha mlipuko wa magonjwa,” amesema Mkongo.
Pamoja na athari za biashara zisizo rasmi, hoja nyingine iliyojitokeza katika kikao hicho ni uchafu uliokithiri na ubovu wa miundombinu ya masoko, hususan Soko la Mawenzi.
Mjumbe wa kikao, Mchungaji Sauli Kajula ameiomba Serikali kuboresha masoko hayo ambayo ni sehemu muhimu ya uchumi wa manispaa.
Baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara nyakati za jioni wamekiri kutambua changamoto za mazingira hayo.
Rahimu Shabani, ameiomba Serikali kuwatengea eneo lenye mzunguko mkubwa wa watu mjini badala ya kuwasogeza mbali, jambo ambalo litafanya biashara zao kuwa ngumu.
“Hapa tulipo mazingira si rafiki, lakini kama Serikali ingetutengea eneo bora, tuko tayari kuhamia. Ombi letu ni tushirikishwe katika maamuzi ya maeneo yatakayopendekezwa,” amesema Shabani.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema tayari fedha za ujenzi wa Soko la Matunda la Mawenzi zipo na kinachosubiriwa ni kuanza kwa ujenzi huo ili kuondoa usumbufu uliopo sasa.
“Wataalamu waliopewa jukumu la kupitia upya mchoro wa ujenzi wa soko hili wafanye haraka ili tuwaondolee adha wafanyabiashara waliopo katika eneo hilo,” amesema Kilakala.
Morogoro ni moja ya mikoa inayoendelea kuwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara wadogo (wamachinga), licha ya juhudi za Halmashauri ya Manispaa kujenga masoko kwa ajili yao.