Mahakama yaamuru mshtakiwa atoe wapangaji aliowapangisha

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru mshtakiwa Madina Bille, aliyekuwa anakabiliwa na shtaka la kuingia kwa jinai katika nyumba ya Zulekha Abdulwahid, kwenda kuwatoa wapangaji aliowapangisha ndani ya nyumba hiyo mara moja.

Pia, Mahakama hiyo imemuachia huru mshtakiwa huyo kwa masharti ya kutokufanya kosa lolote la jinai ndani ya miezi 12, kuanzia siku ya hukumu ilipotolewa.

Madina alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kuingia kwa jinai katika nyumba ya ghorofa nne, mali ya Zulekha Abdulwahid  kisha kupangisha wapangaji kinyume cha sheria.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo, baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo la kuingia kwa jinai.

Hukumu hiyo imetolewa, leo Jumanne Januari 7, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hakimu Swallo amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka.

Amesema Serikali ilikuwa na jumla ya mashahidi sita waliothibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa, huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wawili.

“Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, mahakama imejiridhisha upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi yao bila kuacha shaka, hivyo Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Swallo.

Amesema Mahakama imethibitisha nyumba hiyo ni mali halali ya mlalamikaji, Zulekha Abdulwahid na mumewe Abdulwahidi Ismail ambaye baada ya kufariki dunia, umiliki ulibaki kwa Zulekha kwa mujibu wa nyaraka kutoka Wizara ya Ardhi.

Akichambua ushahidi wa upande wa utetezi, Hakimu Swallo amesema katika utetezi wake Madina alidai aliruhusiwa na mumewe Abdulwahidi Ismail kuishi katika nyumba hiyo na baadaye alihamishiwa Kurasini.

Madina, alidai yeye ni mke mdogo wa Abdulwahid na kwamba alipewa sehemu ya kuishi katika nyumba hiyo, hivyo aliamua kuwapangisha wapangaji hao ghorofa ya nne.

Alidai, baada ya mume huyo kufariki dunia, familia haikufuatilia suala la kugawana mali wala kufungua mirathi.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana shtaka linalomkabili, lakini hakubisha suala la kuwapangisha wapangaji katika nyumba hiyo.

“Mshtakiwa hakuwasilisha mahakamani uthibitisho wowote wa umiliki wake katika nyumba hiyo, ni wazi kwamba aliingia kwa jinai,” amesema Hakimu.

Awali, kabla ya kutolewa hukumu, Wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru ameomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kutokana na kitendo alichokifanya kuwa ni kinyume cha sheria.

Pia, wakili Mzamiru aliomba Mahakama itoa hati ya kuwaondoa wapangaji waliopangishwa na Madina katika nyumba ya Zulekha.

Kwa upande wake, mshtakiwa kupitia wakili wake Moses Kalowa aliomba Mahakama impe adhabu ndogo mteja wake kwa kuwa, ni mgonjwa na hata wakati wa usikilizwaji wa kesi yake alikuwa anawasilisha mahakamni nyaraka mbalimbali za hospitali alikokuwa anahudhuria kwa ajili ya matibabu na vipimo.

Wakili Moses amedai mteja wake anategemewa na mama yake mzazi ambaye ni mtu mzima.

Hakimu Swallo katika hukumu yake baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, amesema amezingatia maombi ya pande zote mbili kwamba mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na pia shauri hilo linahusisha mambo ya kifamilia.

Pia, amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka la Mahakama hiyo kutoa hati ya kuwaondoa wapangaji waliopangishwa na Madina.

“Kutokana na maombi yaliyowasilishwa pande zote, Mahakaka inakuhukumu kutofanya kosa lolote la jinai ndani ya miezi 12 kuanzia leo,” amesema Hakimu Swallo na kuongeza.

“Pia, Mahakama hii, imetoa hati ya kuwaondoka wapangaji waliopangishwa na mshtakiwa huyu na kwamba Madina unatakiwa kwenda kuwatoa wapangaji wako aliowapangisha ndani ya nyumba hiyo mara moja,” amesema Hakimu

Katika kesi ya msingi, Madina alikuwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Novemba 2015 hadi April, 2022, katika Mtaa wa Lumumba uliopo Kariakoo, Wilaya ya Ilala.

Inadaiwa katika kipindi hicho, Madina aliingia kwa jinai katika nyumba namba 23 kitalu 74 mali ya Zulekha Abdulwahid, wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Iliendelea kudaiwa kwamba, mshtakiwa baada ya kuingia katika nyumba hiyo, alipangisha mtu, wakati akijua sio nyumba yake.

Hata hivyo, Desemba, 2023 mshtakiwa huyo alikamatwa na kupelekwa kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam na kuhojiwa kwa tuhuma hizo na baadaye alifikishwa mahakamani hapo kujibu tuhuma zinazomkabili.

Related Posts

en English sw Swahili