WAKATI michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu 2025 ikishirikisha timu za taifa kwa mara ya kwanza, kikosi cha Kilimanjaro Stars kimejikuta kikiweka rekodi mbovu.
Hatua hiyo imekuja baada ya leo Januari 7, 2025 kupoteza mchezo wa pili mfululizo dhidi ya Kenya kwa mabao 2-0.
Mbali na kupoteza mchezo huo, pia ndiyo timu pekee ambayo haijafunga bao wala kupata pointi yoyote baada ya kucheza mechi mbili sawa na wenzake. Kabla ya hapo, ilianza kwa kufungwa 1-0 na Zanzibar Heroes.
Katika mchezo wa leo uliochezwa Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kutofungana huku kila upande ukisaka ushindi wa kuwaweka sehemu nzuri ya kuisaka fainali.
Kipindi cha pili dakika ya 56, krosi iliyopigwa kutoka upande wa kushoto mwa lango la Kilimanjaro Stars, walinzi walishindwa kukaa imara kuondoa hatari hiyo, ikatoa nafasi kwa Boniface Muchiri kufunga bao na kuipa uongozi Kenya.
Kuingia kwa bao hilo, kulilifanya benchi la ufundi la Kilimanjaro Stars linaloongozwa na Kocha Mkuu, Ahmad Ally kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili dakika ya 59 kwa kuwatoa Semfuko Charles na Ofen Chikola huku nafasi zao zikichukuliwa na Hija Shamte na William Edgar.
Licha ya kuingia kwa wachezaji hao, bado Kilimanjaro Stars haikuwa na mashambulizi ya kutisha langoni mwa Kenya na kumfanya kipa Farouk Shikhalo muda mwingi kubaki huru.
Dakika ya 68, Ryan Ogam aliyatumia vizuri makosa ya beki wa Kilimanjaro Stars, Edson Katanga aliyeurudisha mpira ambao haukufika kwa kipa Metacha Mnata aliyeteleza, akaifungia Kenya bao la pili.
Juhudi za Kilimanjaro Stars kusawazisha mabao hayo ziliendelea ambapo yalifanyika mabadiliko mengine kwa kuingia Sabri Kondo na Joshua Ibrahim kuchukua nafasi ya Ayoub Lyanga na Idd Seleman. Hata hivyo, hadi filimbi ya mwisho inapulizwa matokeo yalibaki kuwa Kenya 2-0 Kilimanjaro Stars.
Kilimanjaro Stars kupoteza mchezo huo inamaanisha kwamba haina nafasi ya kucheza fainali hata kama itashinda mechi ya mwisho itakayocheza Januari 9, mwaka huu dhidi ya Burkina Faso kwani ushindi kwao itawafanya kupata pointi tatu.
Kwa sasa msimamo wa michuano hiyo inayoshirikisha timu nne unaonyesha Kenya inaongoza kwa tofauti ya mabao ikiwa na pointi nne sawa na Burkina Faso, ikifuatiwa na Zanzibar Heroes yenye pointi tatu huku Kilimanjaro Stars haina kitu baada ya zote kucheza mechi mbili.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ahmad Ally, amesema: “Umakini mdogo ndiyo umesababisha tumeruhusu mabao mawili leo, ni kweli kuna makosa yamefanyika ndiyo maana imetugharimu.
“Wakati mwingine inatokea unaweza kuwa na wachezaji wote wazuri na ukapoteza, huu ni mchezo. Leo ni siku mbaya kwetu.”
Kwa upande wa Kocha wa Kenya, Francis Kimanzi, amesema: “Nadhani ni usiku mzuri kwetu, tulijiandaa vizuri kuhusu kwenda hatua inayofuata, ni matokeo mazuri sana kwetu.
“Kilichobaki sasa ni kwenda kufanya vizuri zaidi mchezo unaofuatia dhidi ya Zanzibar Heroes ili kufikia malengo ya kucheza fainali na kuwa mabingwa.”
Baada ya mchezo wa leo kumalizika, kesho Jumatano Januari 8, 2025 ni mapumziko, kisha michuano hiyo itaendelea Januari 9 kwa mchezo baina ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Burkina Faso, huku Januari 10 ikiwa zamu ya Zanzibar Heroes na Kenya. Mechi zote zitachezwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Timu mbili zitakazokuwa na pointi nyingi zitacheza fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Januari 13 mwaka huu.