Njia ya ndege yasitisha ujenzi mnara wa mawasiliano Uru, wananchi waja juu

Moshi. Wananchi wa Kata ya Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kusitishwa kwa  ujenzi wa mnara wa mawasiliano uliokuwa unajengwa, hali inayowafanya kuendelea kuishi katika mazingira magumu ya kukosa mawasiliano ya simu katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.

Changamoto ya mawasiliano katika kata hiyo  inadaiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 10, hali inayoathiri mifumo ya biashara ikiwamo ile inayotumia miamala ya kifedha na mifumo ya intaneti kwa ujuma.

Mradi huo ulioanza Desemba mwaka jana, ulitarajiwa kukamilika Februari mwaka huu, lakini baada ya kuchimbwa msingi na vifaa kuwekwa eneo la mradi kuendelea na kazi, Januari 3, 2025 vifaa hivyo viliondolewa kwa madai kuwa eneo hilo ni njia ya ndege.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Peter Mwasalyanda ambaye amesema walipaswa kujenga mnara wa mita 50 katika eneo hilo, lakini baada ya kuomba kibali Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCIAA) imewajulisha kuwa hawataweza kuendelea na ujenzi huo kutokana na sababu za usalama wa anga.

“Utaratibu wa ujenzi wa miradi sehemu yoyote unahitaji kupata vibali na mmoja wa taasisi za kutoa vibali ni TCIAA, kwa hiyo unapojenga kitu kirefu kwenda angani lazima watoe kibali.

“Sasa pale Uru Shimbwe tulitaka kujenga mnara wa mita 50 na walishaanza maandalizi ya kuchimba shimo la msingi wakitegemea kwamba kibali kitatoka na mnara hautakuwa na shida, lakini TCIAA  wametujulisha kwamba  kwa maeneo hayo hawashauri mnara wa mita hizo ujengwe kwa sababu ya usalama wa anga.”

Amesema kwa sasa makandarasi wameanza upya kazi ya usanifu ili kuona ni mnara wa urefu gani unaoweza kutosheleza.

Mwasalyanda amesema kama utajengwa eneo hilo, utakuwa mfupi na hautafika mita 50.

“Unaweza kuwa mita 30 lakini lazima tuangalie kama ni mfupi, je tutapata ile line of site, maana minara  lazima ionane,” amesema ofisa huyo.

Hivyo hivyo,  amewaomba wananchi wawe na subira, kama watakubaliana, mnara utajengwa mfupi kidogo lakini kama itashindikana hilo kutokana na muongozo wa TCIAA watalazimika kutafuta eneo lingine ndani ya kata hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, leo Jumanne Januari 7,2025, wananchi wa kata hiyo, wamesema kusitishwa kwa ujenzi wa mnara huo kumeibua taharuki na kuwaacha njia panda kwa kuwa, hawajaelezwa sababu za kusitishwa kwa ujenzi huo.

Liberatus Tesha, mkazi wa Kitongoji cha Kowere, Kijiji cha Shimbwe Juu amesema mradi huo wa mnara ulikuwa ukitekelezwa na Serikali kwa ajili ya kumaliza changamoto ya mawasiliano, kusitishwa kwa ujenzi huo kumewaacha katika giza nene.

“Kero yetu kubwa ni kuona mradi ambao tulipewa na Serikali ukisitishwa bila kupewa taarifa ni nini kinaendelea, tumeachwa njiapanda,”amesema Tesha.

Naye Lucy Akaro amesema waliamini kuanza kwa ujenzi wa mnara huo ndiyo itakuwa tamati ya adha ya mtandao, lakini matumaini yao yameyeyuka ghafla baada ya kutaarifiwa kuwa ujenzi umesitishwa.

“Tuliletewa mradi huu ili kuturahisishia huduma za mawasiliano, wananchi tunateseka sana, hata watoto wakitutumia hela kwenye simu kuzitoa ni gharama maana tunalazimika kwenda Mjini Moshi ambako nauli ni zaidi ya Sh5,000 ili kutoa Sh10,000 tuliyotumiwa, hii ni changamoto, serikali iingilie kati hili,” amesema Akaro.

Aisimbo Venance amesema, “changamoto yetu kubwa ni mawasiliano ya simu, watoto wetu wengine wanasoma shule mbali, wakati mwingine wanapata shida wanashindwa kuwasiliana na wazazi ili wapate msaada kutokana na kukosekana kwa mawasiliano, wakati mwingine unataka kumtumia hata hela unashindwa hadi uende Moshi mjini, niomba Serikali huu mradi usisimame tumeteska kiasi cha kutosha.”

Remmy Severine, mkazi wa Kijiji cha Shimbwe Juu aliyekuwa akilinda vifaa vya ujenzi wa mnara huo, amesema alikabidhiwa vifaa hivyo Desemba 16, 2024, kutoka kwa wahandisi waliokuwa wanajenga mnara na vilichukuliwa Januari 3, 2025, baada ya kuambiwa kuwa mradi huo umesitishwa hadi vitakapopatikana vibali kutoka kwa mamlaka ya anga.

Wenyeviti, diwani, mkandarasi, wazungumza

Mwenyekiti wa Kijiji cha Shimbwe Chini, Alexander Temba amesema ujenzi wa mnara huo ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali na mwaka jana wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa,  ilionyesha nia ya kuujenga na mwezi uliopita ujenzi ulianza.

“Mhandisi na mkandarasi walikamilisha mikataba ya ujenzi na kazi ikaanza, wamechimba msingi ambao sasa umekuja kuwa kama kaburi na kuleta baadhi ya vifaa kwa ajili ya msingi huo lakini vimeshaondolewa,” amesema Temba.

Hata hivyo, ameshangaa kuona ujenzi ukisitishwa bila taarifa kamili ya kipi kimetokea.

“Tumeachwa njiapanda, hatuelewi kinachoendelea. Mwaka huu tena kuna uchaguzi na hatujui tutawaambia wananchi nini, maana kama mnara huu hautakamilika kwa wakati, sidhani kama watapiga kura,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Shimbwe Juu, Elandinga Uwoya amesema baada ya kupata taarifa kuhusu kuondolewa kwa vifaa vya ujenzi wa mnara, alimfuata mkandarasi ili kujua kuna shida gani akajibiwa kuwa mamlaka ya anga imezuia ujenzi huo kwa sababu eneo hilo ni njia ya ndege.

“Wananchi wa Shimbwe wanahisi kutapeliwa, kwa muda mrefu wanapitia hali ngumu, mawasiliano na Serikali ni duni, tunateseka, tunataka Serikali itazame hili kwa jicho la huruma,” amesema.

Diwani wa Uru Shimbwe, Bertin Mkami amesema mradi huo ulitakiwa kukamilika ndani ya siku 90 baada ya mkataba kusainiwa, lakini baadaye vifaa viliondolewa bila kushirikisha viongozi wa kata na vijiji.

“Baada ya mkandarasi kuanza kazi Novemba, tulianza kutafuta vibali na baadaye alisaini mkataba kwa kazi ya siku 90. Alianza kuchimba msingi na kuleta vifaa, lakini ghafla walikuja kuchukua vifaa bila kushirikisha viongozi wa kata au vijiji. Walidai wamesimamishwa na mamlaka ya anga,” amesema Mkami.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hilo, mkandarasi mdogo wa mradi huo, Seleman Nyambaya amesema kazi ya ujenzi imekoma kwa sasa kutokana na maelekezo kutoka kwa mkandarasi mkuu aliyewaambia wanasubiri kibali kutoka kwa mamlaka ya anga.

“Hii ni miradi ya Serikali na inatekelezwa kwa kufuata utaratibu. Kama mkandarasi mdogo, tumechukua vifaa baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa mkandarasi mkuu kwamba mradi umesitishwa hadi kibali cha mamlaka ya anga kitakapotolewa. Mara kibali kitakapotoka, tutarudi kuendelea na mradi,” amesema Nyambaya.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amesema tayari amefuatilia suala hilo na kupewa taarifa kuwa mradi huo umesitishwa baada ya kubainika kujengwa kwenye njia ya ndege na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati mamlaka zinashughulikia suala hilo.

“Taarifa nilizo nazo ni kwamba mradi ule wa mnara umesitishwa na mamlaka ya anga kwa sababu ulikuwa unajengwa kwenye njia ya ndege na kitaalamu haitakiwi kujengwa mnara ambako ndege zinapita mara kwa mara,” amesema Profesa Ndakidemi.

Amewatoa hofu wananchi hao akisema mradi huo utabaki kuwa ni wa Uru Shimbwe, utahamishiwa eneo lingine katika kata hiyo na kazi ya ujenzi itaendelea kama ilivyokuwa imepangwa.

“Tayari nimewasiliana na waziri husika amenihakikishia hakuna kitakachoharibika na niombe wananchi wawe watulivu kila kitu kitakwenda sawa,” amesema mbunge huyo.

Related Posts