Iringa. Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji inayowakabili viongozi watano wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo umeieleza Mahakama ya Wilaya ya Iringa kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga, Diwani wa Nyanzwa, Boniface Ugwale, Katibu wa mbunge wa Kilolo, Kefa Walles, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mlandege, Wille Chikweo na Silla Kimwaga.
Wanakabiliwa na kesi ya mauaji wakituhumiwa kumuua aliyekuwa Katibu wa chama hicho Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki (56).
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo nyumbani kwa Kibiki eneo la Banawanu, Kata ya Mseke, Novemba 12, 2024 usiku kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka katika kesi ya jinai namba 34404 ya mwaka 2024.
Kesi hiyo imetajwa mahakamani leo Jumanne, Januari 7, 2025 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Sauli Makori ameieleza Mahakama kuwa, upelelezi unaendelea, hivyo ameomba Mahakama itoe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Ombi hilo halikupingwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rehema Mayagilo anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hii ya awali. Kesi imeahirisha kwa siku 14 hadi Januari 21, 2025.
Washtakiwa wanaowakilishwa na mawakili wa kujitegemea Barnabas Nyalusi na Neema Chacha wamerejeshwa mahabusu kwa kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo katika hatua ya usikilizwaji wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji ikiwa ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kisheria.