Samwasa kusambaza maji kwa wakazi wa Kavambughu, Mahuu

Same. Wakazi 5,600 wa vitongoji vya Kavambughu na Mahuu wilayani Same, Kilimanjaro wameanza kupata huduma ya majisafi na salama baada ya Mamlaka ya Maji Same (Samwasa) kutekeleza mradi wa kuendeleza mtandao wa maji kwenye maeneo ya vitongoji.

Mradi huo mkubwa wa maji unaohudumia wilaya za Same na Korogwe, Tanga awali ulimfanya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuweka kibarua chake rehani kama usingekamilika kwa wakati ili wananchi wapate majisafi.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilida Mgeni ametembelea mradi huo leo Jumanne, Januari 7,2025 kujionea maendeleo ya mradi huo na kusema tatizo la maji lilikuwa kubwa, lakini kwa sasa maji yanatoka na wananchi wanapata huduma.

“Kuja kwangu hapa nimekuja kujihakikishia kama maji yanatoka, maana wiki mbili zilizopita nilikuja na Naibu Waziri wa Maji, Methew Kundo na akatoa maagizo kuwa ndani ya wiki mbili maji yatoke  katika vitongoji hivi na leo yanatoka,” amesema Mgeni ambaye pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali huku akiwataka wananchi kulinda mradi huo kwa manufaa ya vizazi na vizazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Samwasa, Rashid Mwinjuma amesema mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 95 huku jumla ya vituo sita vya maji kwenye vitongoji hivyo vikipata huduma ya maji.

“Azma ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani na sisi Samwasa tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunatimiza azma hiyo,” amesema Mwijuma.

Amesema Samwasa inaendelea kutekeleza miradi mingine zaidi ya minane ndani ya mji wa Same yenye thamani ya Sh200 milioni ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inasogeza huduma za maji karibu na wananchi.

Amesisitiza kuwa, kukamilika kwa mradi huo, kutawezesha wakazi wa vitongoji hivyo kupata maji kwa gharama nafuu pamoja na kufungua fursa zingine za kiuchumi.

“Kwa sasa mamlaka imepokea maombi 276 ya wakazi wa Mahuu wanaotaka kuunganishiwa maji na tayari maombi 162 wameshapatiwa kumbukumbu namba kwa ajili ya malipo,” amesema Mwinjuma.

Awali, wananchi wa vitongoji hivyo walisema tangu kupata Uhuru hawajawahi kupata maji ya bomba kama ilivyo kwa sasa na kwamba, wanaipongeza Serikali kwa kutimiza ahadi.

“Tulikuwa hatulali tunakwenda kilometa zaidi ya tano kutafuta maji, tulihatarisha maisha na ndoa zetu kwa ajili ya maji. Kwa sasa tunashukuru tunachota maji ndani na nje ya makazi yetu,” amesema mkazi wa Mahuu.

Mwanaidi Mghumi, mkazi wa Kitongoji cha Mahuu, amesema walikuwa wanafuata maji mjini kwa gharama ya Sh500 kwa dumu la lita 20, lakini kwa sasa mambo yamekuwa tofauti kwani hawaendi tena.

Diwani wa Same Mjini, Richard Mrita amesema historia imeandikwa katika vitongoji hivyo kwa kupata maji na kwamba, changamoto hiyo ilikuwa inamnyima usingizi kwa wananchi kupata shida kila kukicha.

Related Posts