NIKWAMBIE MAMA: Tatizo la ajira litufunze kujiajiri

Siku moja Mtemi Kimweri aliota ndoto ya kutisha sana. Ndotoni aliona watu weupe kama karatasi wakiteremka mashuani, wakaingia kwenye ardhi yake na kuanza kuyapinga yote yaliyofanyika chini ya Mtemi. Walipita madarasani na kuiponda elimu yao, wakapita kwenye burudani na kuziponda ngoma zao. Hata kwenye nyumba za ibada walizikandia imani zao kwa kusema mambo yote waliyofuata yalikuwa batili.

Ikumbukwe kuwa wakoloni walipotaka kumharibia Mwafrika walimtawala kiimani, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi. Walimlazimisha elimu tofauti ambayo haikumtosheleza kujikomboa na kujitegemea. Mwisho wa siku wazalendo walikuwa tegemezi na walibaki wakifuata kila walichoelekezwa na mabwana wao. Walipofanya kazi haikuwa kwa manufaa yao, bali walifanyishwa kazi kwa faida ya watawala.

Baada ya kutumikishwa vya kutosha, wazalendo waliungana kwa siri kupitia vilabu vya michezo na burudani. Wakapanga mikakati na hatimaye wakajikomboa kutoka utumwani. Walianza kama waliokwenda kushiriki michezo na burudani, kumbe walikuwa na jambo lao, wakielimishana namna ya kujikwamua kutoka kwenye makucha ya ukoloni. Kwa njia hii ilikuwa vigumu kwa watawala kuwabaini mapema.

Baada ya kujikomboa, Mwalimu Nyerere alikuja na “Elimu ya Kujitegemea” iliyowainua hata wale wazalendo waliokosa elimu pale mwanzoni. Katika kusisitiza hilo, kila mtoto aliyefika au kuvuka umri wa kwenda shule alisajiliwa. Pia, ikaanzishwa elimu ya Ngumbaru waliyopewa watu wazima. Papo hapo ikaja mifumo ya Chipukizi, Skauti na Jeshi la Kujenga Taifa kwa nia ya kukuza uzalendo na kuondoa chembechembe za utwana.

Uzalendo ulianza kufundishwa kwa mtoto tangu akiwa shule ya msingi. Kuna ukweli kuwa mtoto hushika mambo anayoelekezwa kwa ukamilifu zaidi ya mtu mzima. Ndiyo maana mtoto anayefunzwa mpira anakuwa mahiri zaidi ukubwani kulinganisha na mchezaji aliyeibukia ukubwani. Mtoto huyu alipohitimu na kuwa tayari kulitumikia Taifa, alipitishwa kwanza kwenye Jeshi la Kujenga Taifa ili kumtia ukakamavu na uzalendo dhidi ya uvivu na ufisadi wa mali ya Taifa lake.

Hapo ndipo tofauti ya waliokuwa nguvukazi ya Taifa wa enzi zile inapoonekana wazi ukilinganisha na vijana wa leo. Hata sasa huku mtaani tunao wazee wastaafu walioingia kwenye sekta binafsi. Wazee hawa wanatofautiana sana na vijana wa kizazi kipya kwenye weledi wa kazi. Kama wangelikuwa na nguvu na kasi kama walivyokuwa katika enzi zao, sidhani kama vijana wangeonekana kwenye soko la ajira.

Ninachotaka kusema ni umuhimu wa Elimu ya Kujitegemea. Hivi sasa dunia inahangaika na soko la ajira. Vijana walio kwenye foleni ya ajira ni wengi kuliko ajira zilizopo Serikalini na kwenye sekta binafsi. Lakini kama hilo halionekani, mifumo yetu inaendelea kuingiza maelfu ya vijana kila mwaka wa uhitimu kwenye msururu wa kusaka ajira bila kujali hatima yao. Matokeo yake ni kuzalisha wahalifu, waraibu na wafanyabiashara haramu.

Katika hatua ya kushangaza, Serikali inawaelekeza vijana hawa waache kuhangaikia kuajiriwa na badala yake wajiajiri. Suala gumu ni kwamba kujiajiri kunahitaji elimu na maandalizi. Pengine tunaona jinsi wenzetu akina Bill Gates wanavyoitingisha dunia kwa kujiajiri na kuajiri wenzao, lakini je, tumewatayarisha Bill Gates wangapi hapa nchini? Au tunadhani wanashuka kutoka mbinguni?

Kule Uingereza kuna mfuko uliosaidia vikundi vya watu 40 unaoitwa “Unemployed Benefitable 40”. Kikundi cha watu 40 wasio na ajira waliweza kujaza fomu na kupata mtaji na mwongozo wa matumizi ya mitaji. Mfuko huu umesaidia wengi, wakiwemo wakulima, mafundi, wanamitindo na wasanii, wakiwemo wanamuziki maarufu duniani “UB40”. Utaratibu ulikuwa ni kujaza fomu na kuikabidhi kwa wahusika.

Sikatai kwamba hapa tunayo mifuko kuanzia kwenye majimbo inayowakopesha vijana, akina mama na watu wa makundi maalumu. Lakini bado kuna shida kwenye mifuko hiyo. Vilevile, elimu ya kutosha ya namna ya upatikanaji wa mitaji kutoka humo bado haijasambazwa kwa walengwa. Hapa nina maana saikolojia ya mlengwa inakuwa imeganda kwenye kufaulu mtihani na kuajiriwa. Hakuna anayesomea kujiajiri.

Hakuna yeyote anayeweza kujiajiri bila kujua anakwenda kujiajiri kwenye mrengo upi. Kijana aliyesomea udaktari siye aliyesomea namna ya kuanzisha na kuendesha kituo cha afya. Isitoshe hawezi kuamka na mtaji kutoka kwenye familia zetu masikini. Bado mambo ni magumu kwa wanaotoka vyuoni na kuanza kujiajiri bila kuanza kuajiriwa na taasisi zisizokuwepo.

Kwa maoni yangu, Elimu ya Kujitegemea irudishwe kwenye mtalaa. Yapo masomo mengi yaliyofutwa yakingali msaada mkubwa dhidi ya tatizo la ajira. Kwa mfano stadi za kazi, sayansi kimu na mengineyo yalikuwa na umuhimu wake kwa wajasiriamali. Hata vile vitabu vya “Mahali Pasipo na Dakitari” vilipofundishwa kwenye shule za msingi vilikuwa msaada mkubwa kwa wakunga baadaye.

Lengo la Elimu ya Kujitegemea ni kupambana na maadui watatu; ujinga, umasikini na maradhi. Elimu hii humpa mwanafunzi ujasiri wa kujiajirim kwani anatoka akiwa na ujuzi. Na tunakubaliana kuwa tukiwashinda maadui hawa, tutakuwa na hali bora. Tofauti na maneno ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kiimani kwamba kuwategemea wao ndio kushinda. Ni lazima sasa tubadilike na kuacha kutumbukia kwenye korongo walilokwisha kutumbukia wengi.

Related Posts