Mvua yaacha kilio Kahama, makazi yaharibiwa

Kahama. Mvua iliyonyesha wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga imeleta athari katika baadhi ya maeneo, ikijaza mitaro ya majitaka na kufurika katika makazi ya watu.

Wakizungumza na Mwananchi jana Januari 7, 2025, baadhi ya wananchi wa Kata ya Mulanga na Majengo wilayani hapa wamesema maji hayo yamewakosesha makazi, kuharibu mali na kuhatarisha afya zao.

Kuruthumu Dafa mkazi wa Kata ya Majengo amesema kuwa ni athari kubwa wanazokumbana nazo kutokana na maji ya mvua maji machafu yanaingia ndani na maji kiasi cha kufikia madirishani.

“Maji ya mvua yanakuja hadi katika makazi yetu mengine yana kinyesi na uchafu mwingi na kuna wakati hadi nyoka wanaingia ndani, tunaomba Serikali itusaidie sisi hatuna pa kwenda,” amesema Kuruthumu.

Bernadetta Damas amesema kuwa changamoto ni mtaro ambao haukuwepo awali walipokuwa ananunua eneo hilo na baada ya kupitsha huo mtaro kumekua na changamoto kama hizi.

“Awali huu mtaro haukuwepo lakini baada ya kupitishwa huu mtaro kumekuwa na changamoto maji yenye vinyesi yanapita, takataka zote hadi nyoka tunakuwa kama wakimbizi na hatuna amani wakati maeneo ni ya kwetu magodoro, makochi yameloana na TV haifanyi kazi, maji yameingia ndani,” amesema Damas.

Akizungumzia kero hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amesema, athari hizo zimesababishwa na uborashaji wa mji kupitia mradi wa uboreshaji miji (Tactics) katika Manispaa ya Kahama.

“Katika Kata za Mulanga na Majengo kumetokea athari hii kwa sababu kuna mradi wa uboreshaji miji katika wilaya yetu, ambapo pia kuna uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya ujenzi wa barabara na hizi mvua zimekua zikinyesha kwa muda mrefu hasa nyakati za usiku.

“Tulichofanya ni kuhakikisha wakandarasi na Tarura (Wakala wa Barabara Mijini na Vijini) wako huko kurekebisha hilo na kuhakikisha na pia kasi a ujenzi inaongozeka ili kukamilisha haraka,” amesema Mhita.

Kaimu meneja wa Tarura Wilaya ya Kahama, Masola Juma amethibitisha kutokea kwa athari hizo kwa baadhi ya kata ambazo zimesababishwa na mvua zilizonyesha mfululizo na kuharibu barabara na kusababisha maji kwenda kwa wananchi,

 “Hatua ya awali tunayochukua ni kuhakikisha mkandarasi anakwenda kuzuia yale maji kwa haraka yasielekee katika makazi ya wananchi ili mvua zitakazo endelea zisirudie kuathiri hayo maeneo.

“Pia tunatembelea madaraja na mitaro yote ktoa uchafu uliokwama na pi tunatoa wito kwa wananchi kutokufanya mitaro sehemu ya kutupa taka,” amesema Juma.

Related Posts