Dar es Salaam. Sista Inah Canabarro Lucas raia wa Brazil anatajwa kuwa ndiye mtawa mwenye umri mkubwa zaidi duniani kwa sasa baada ya kifo cha Tomiko Itooka wa Japan aliyefariki akiwa na miaka 116.
Inah (116) alizaliwa Juni 8, 1908, huko São Francisco de Assis, Rio Grande do Sul, Brazil. Alipokea nadhiri zake za kitawa mwaka 1934 na akatumika kama mwalimu wa lugha ya Kireno na Hisabati katika miji mbalimbali ya Brazil.
Miongoni mwa wanafunzi wake mashuhuri alikuwa General João Figueiredo, ofisa wa kijeshi na mwanasiasa wa Brazil ambaye alihudumu kama Rais wa 30 wa Brazil kuanzia 1979 – 1985. Alikuwa rais wa mwisho wa utawala wa kijeshi uliotawala Brazil kutoka 1964 hadi 1985.
Hata hivyo ukiachana na maisha ya utawa pia ni mpenda soka na shabiki mkubwa wa timu ya soka ya Sport Club Internacional. Kila mwaka, timu hiyo humuenzi kama shabiki wao mzee zaidi duniani.
Itakumbukwa Papa Francis alimpa baraka ya kitume wakati akisherehekea kutimiza miaka 110 mwaka 2018.
Mnamo Machi 2024, Inah aliiambia ACI Digital kwamba moja ya siri za maisha yake marefu ni sala: “Ninasali rozari kila siku kwa ajili ya kila mtu duniani.”
Wakati mtawa huyo akitimiza umri huo, kwa Tanzania yupo Padri Luois Shayo wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mwafrika wa kwanza kuwa Paroko wa jimbo kwa sasa ana miaka 105.
Padri Luois wakati akizungumza na Mwananchi alisema kuishi kwake ni siri ambayo Mungu ameificha katika maisha yake.
Alisema amevuka milima na mabonde katika safari yake ya utume, lakini bado ana afya njema, jambo analomshukuru Mungu.
Padri huyo ambaye pia ni mwafrika wa 16 kupata upadri mwaka 1950, Juni 30, mwaka jana alitimiza miaka hiyo 105 na miaka 74 ya upadri na huenda akavunja rekodi ya kuwa padri aliyeishi miaka mingi zaidi Barani Afrika.
Padri huyo ni miongoni mwa watoto tisa kwenye familia ya mzee Shayo wa Kijiji cha Imii, kilichopo Kilema wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na kwa sasa anaishi katika nyumba ya mapadri wazee Longuo.