HESABU za Yanga hivi sasa ni kushinda mechi zao mbili zijazo za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal (ugenini) na MC Alger (nyumbani) ili wafuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Yanga inapiga hesabu hizo bila ya kuangalia MC Alger na TP Mazembe watafanya nini katika mechi zao kwani ndiyo timu zinazowania nafasi moja ya kufuzu robo fainali kutoka Kundi A baada ya Al Hilal kutangulia.
Kutokana na hilo, Mwanaspoti limepenyezewa kwamba bosi wa klabu hiyo, Gharib Said Mohamed (GSM) kuwaahidi mastaa wa kikosi hicho kiasi cha shilingi milioni 500 kama wataichapa Al Hilal na MC Alger.
Ahadi hiyo ilitolewa baada ya Yanga kuichapa TP Mazembe mabao 3-1 katika mchezo uliopita uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kufufua zaidi ya kufuzu robo fainali kutokana na kufikisha alama nne. Vinara Al Hilal waliotangulia robo fainali wana alama 10, MC Alger (5) na TP Mazembe (2) wakiburuza mkia.
Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa, mastaa wa Yanga wamewekewa ahadi hiyo endapo wakishinda mechi hizo mbili zilizobaki na kutinga robo fainali ambapo itakuwa ni mara ya pili mfululizo kufanya hivyo baada ya msimu uliopita walipokuwa wakifundishwa na Miguel Gamondi.
“Bosi mwenyewe (GSM) ndiye amewaahidi kiasi hicho cha fedha shilingi milioni 500 kama bonasi yao, hivyo lazima wapambane ili kuvuna alama sita ugenini na nyumbani,” kilisema chanzo hicho.
Ni wazi kuwa, mastaa wa Yanga watakuwa na wakati mgumu katika mechi hizo wakianza dhidi ya Al Hilal licha ya kwamba kocha wa Wasudan hao wenye maskani yao Mauritania, Florent Ibenge kusema atabadilisha kikosi kwa kupumzisha majembe yake. Mchezo wa kwanza Yanga ilikutana na kipigo cha mabao 2-0 nyumbani.
Jumapili ya wiki hii Yanga itakuwa ugenini kukabiliana na Al Hilal katika mchezo unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Cheikha Ould Boadiya uliopo Nouakchott nchini Mauritania kuanzia saa 4:00 usiku.
Baada ya hapo, Yanga itarejea nyumbani kumalizana na MC Alger kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Januari 18 ukiwa ni mchezo wa mwisho wa Kundi A.
Kabla ya Yanga haijacheza dhidi ya Al Hilal, kule Algeria wenyeji MC Alger watawakaribisha TP Mazembe, mechi ikichezwa Ijumaa wiki hii. TP Mazembe itamalizia nyumbani dhidi ya Al Hilal siku moja ambayo pia Yanga itakuwa ikicheza na MC Alger. Baada ya hapo, itafahamika nani ataungana na Al Hilal kufuzu robo fainali kutoka Kundi A la michuano hiyo.