Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kama sekta ya bima nchini itaendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na weledi, nchi itaendelea kufurahi matunda yake.
Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma za bima nchini kusudi waweze kufanyakazi zao katika mazingira rafiki.
Makamu wa Pili, Abdulla aliyasema hayo jana Jumanne Januari 7, 2025 mjini Unguja alipokuwa akipokea hundi ya Sh321 milioni kuunga mkono maadhimisho ya 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyotolewa na Tira na wadau wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI).
Ametoa wito kwa kampuni za bima nchini kuchangamkia fursa za biashara zinazotokana na miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa Zanzibar huku akisema ofisi ya Makamu wa Pili wa Rias iko tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika kwao.
Akizungumzia mchango uliotolewa na Tira na washirika wake, Abdulla amesisitiza kuwa una thamani kubwa na utaelekezwa kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa.
Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Khadija Said alisema mchango huo walioutoa ni moja ya hatua ya utekelezaji wa ahadi ya sekta ya bima nchini ya kuwa sehemu ya maadhimisho hayo.
Amesema lengo ni kutaka kuibua na kuchochea ushirikiano wenye tija na Serikali hususani kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini wakilenga kuona namna kampuni za bima nchini zinavyoweza kushiriki kwenye kukinga majanga.
Mwakilishi wa Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI), Wilson Mnzava ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB (CIC), ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikisha kampuni za Bima katika tukio hilo muhimu.
“Huu ni mwanzo tu, tunaahidi tutaendelea kushiriki kila mwaka ili kuhakikisha sekta ya bima nchini inakuwa miongoni mwa mafanikio ya maadhimisho haya,” amesema Mnzava.
Hata hivyo, ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kutoa fursa kwa kampuni za bima zinazomilikiwa na wazawa kushiriki miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini ile ya serikali na wawekezaji binafsi.