Japo makala zangu zinajikita zaidi kwenye mada za kikatiba, kisheria na haki, lakini mara mojamoja pia ninaingia kwenye mada za kisiasa, kiuchumi na kijamii, mada yangu ya leo, ni ya kuwafundisha Watanzania uzalendo, ingekuwa ni zamani ningewafundisha waandishi wa habari, lakini ujio wa mitandao ya kijamii, sasa kila mtu ni mwandishi.
Uzalendo ninaoufundisha hapa ni uzalendo kuhusu kusema ukweli, kuandika ukweli au kutangaza ukweli, sio lazima kuusema kila ukweli unaousikia, ukimya pia ni busara.
Uzalendo ni kwanza tuwe huru kuusikia ukweli wowote tunaousikia kutoka popote, lakini siyo lazima kuusema kila ukweli unaousikia kwa sababu kuna ukweli mwingine ukisikika, unaweza kuleta sintofahamu zaidi kwa jamii, hivyo ni bora usingesikika kuliko kusikika na kuwachanganya watu.
Ukiusikia ukweli wowote, kabla ya kuusema, kwanza jiulize, je, ni lazima useme kila kitu tunachokisikia au kwanza tutangulize mbele uzalendo na masilahi ya taifa kwa kujiuliza hicho unachotaka kusema kina masilahi kwa taifa?
Na unatakiwa kuupima kwanza huo ukweli kwa kujiuliza, je, ukweli huu ukijulikana una matokeo gani kwa taifa, ndipo uuseme au uendelee tu na hii tabia ya kusema kila kitu unachokisikia? Ukisikia jambo lolote, wewe liseme tu bila kujali jambo hilo lina matokeo gani ilimradi jambo hilo ni la kweli?
Najitolea mfano mimi mwenyewe, kazi yangu kuu ni mwandishi wa habari wa kujitegemea na kanuni kuu ya kwanza ya mwanahabari (cardinal rule) ni “tell nothing but the truth, no matter what”, yaani kazi ya waandishi wa habari ni kuandika au kutangaza ukweli, lakini mwandishi kabla hajaandika au kutangaza, anatakiwa kutumia kitu kinachoitwa “objectivity test”, yaani kuwa na malengo kwa kuupima ukweli huo una faida au manufaa gani kwa jamii, taifa na mhusika?
Ukisikia jambo, ukiambiwa jambo au ukiona jambo, japo ni ukweli lakini kama ukweli huo, ukijulikana, badala ya kujenga, utabomoa, wewe mwandishi unapaswa kuuhifadhi ukweli huo. Huu ndio uzalendo wa kweli wa taifa lako kwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa.
Mimi natoka makabila ya Kanda ya Ziwa, nilifunga ndoa mapema nikiwa kijana wa miaka 25 kwa kumuoa msichana niliyesoma naye, akiwa na umri wa miaka 21.
Kumbe nilioa mapema kabla sijamalizana na ujana, mke wangu akapata fursa ya masomo, miaka minne ya masomo nje ya nchi, huku nyumbani Tanzania, akatokea mdada nikashindwa kuvumilia, nikaanguka dhambini, sisi wakatoliki ukifanya dhambi unaungama kwa padri, dhambi zako zinaondolewa, maisha yanaendelea.
Nilipomtembelea mke Marekani, nikaamua kuwa mkweli, kuusema ukweli kwa wife kuwa ni kweli kuwa sisi Wasukuma kukaa tu miaka minne unamsubiri mtu, hatuwezi, hivyo alisaidiwa. Nikaomba msamaha, nikijua yatakwisha, kumbe kosa. Uliwaka moto, kuuzima nikashindwa mpaka leo mpaka kesho, mume Tanzania, mke Marekani.
Hoja ni kwamba japo ni ukweli na ukweli ni lazima usemwe, lakini kuna ukweli mwingine kabla hujausema, lazima upimwe, kwa kuusema ukweli, je, utajenga? Kwetu sisi wanaume wa Kiafrika, kupiga kona ni kawaida, lakini sijui ni wanaume wangapi wako tayari kuupokea na kuubali ukweli kuwa hata wanawake, wake zetu, nao wana kona zao.
Zingefanywa DNA za watoto wote wa familia zote, kuna familia zingeparaganyika na sijui ni wanaume wangapi wangekubali?
Ni wazi kuwa Tanzania bado tuna demokrasia changa, hivyo kuwekeza katika siasa ni jambo dogo. Lakini ili kupata uungwaji mkono, ni lazima kutangaza kila kitu unachokisikia kuhusu nchi yako? Nchi ni kama nyumba, taasisi ya kwanza ya jamii ni familia, kuna siri za familia, kuna siri za nyumbani, kuna siri za jikoni, kuna siri za chumbani, kuna siri kwenye handbags za wake zetu, kuna siri za vijeluba, kuna siri za simu n.k.
Si busara kila ukweli kuhusu familia yako uutoe nje ya familia, vivyo hivyo na nchi ni kama nyumba, ni kama familia, kuna vitu unaweza kusikia kuhusu nchi yako, na viongozi wake, japo vinaweza kuwa ni vitu vya kweli kabisa, lakini ukiongozwa na uzalendo na utaifa.
Hivyo, kwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa, unaweza kuvisikia vitu hivyo vya kweli kabisa na kuamua kuvikalia kimya, kutovitangaza, kutovisema au kutoviandika, bali kuvifanyia kazi kimya kimya na ukimya huu ndio uzalendo wenyewe.
Japo Rais ni mtumishi wetu, ndiye mkuu wa nchi, ni kama baba wa familia, lazima aheshimiwe akiwa hai au amekufa.
Ni mkuu wetu, pia ni binadamu na sio malaika, shetani anaweza kumfikia, hivyo ana haki ya kutenda makosa na pia ana haki ya faragha yake kuheshimiwa. Si busara kuanika matukio ya faragha za mtu yeyote, akiwa hai au amekufa, tena kumtuhumu mtu aliyetangulia mbele ya haki, na hawezi kujitetea, siyo kumtendea haki. Wito kwa mamlaka husika, hata kama ni kweli, kanusheni ili kumtendea haki marehemu.
Namalizia kwa maswali haya ya msingi; kuhusu hoja za maadili, ni kusema kweli daima, lakini je, ni lazima kuusema kila ukweli unaousikia? Kwenye medani za siasa, kabla ya kuusema ukweli tunaousikia, je, tutangulize kwanza mbele maslahi mapana ya taifa kwa kuupima kwanza, ukweli huo una matokeo gani, ndipo tuuseme, au tuendeleze kusema tu, kupayuka na kuropoka kila ukisikia lolote, uliseme tu kwa sababu ni la kweli?
Wito wangu ni kwamba siyo lazima kusema kila unachosikia, hata kama ni cha kweli, tujifunze kunyamaza, ukimya nao ni jibu.