Ahadi tano za Trump akiingia White House

Zikiwa zimebakia siku 12 za kuapishwa kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, tayari mambo muhimu aliyoyaahidi kwa Wamarekani yanamsubiri ofisini kwake na anatarajiwa kuanza na moja baada ya jingine.

Trump, ambaye ni Rais wa 45 na 47 wa Marekani, anatarajiwa kuapishwa Januari 20, 2025, akichukua nafasi ya Joe Biden, ambaye anamaliza muda wake akiwa ameongoza kwa muhula mmoja pekee wa miaka minne.

Akiwa Rais wa Marekani kati ya mwaka 2016 – 2020, bilionea huyo kupitia kaulimbiu yake ya “Make America Great Again” (Ifanye Marekani Kuwa Juu Tena), aliibua gumzo kupitia hatua alizokuwa akizichukua, ikiwemo kujenga uzio katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Mataifa ya Afrika pia yaliisoma namba, baada ya kukata mirija ya misaada iliyokuwa ikitolewa na taifa hilo lenye nguvu duniani, hususan dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na mabilioni yaliyokuwa yakitolewa kama msaada.

Sasa, kuanzia Januari 20 baada ya kuapishwa, Trump anarejea tena madarakani akiwa na nguvu ya kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Marekani wakati wa uchaguzi na kufanikiwa kumshinda Kamala Harris wa Democrats.

Orodha ya mambo kadhaa iko mbele yake ikimsubiri na alishazungumzia mambo atakayoyafanya muda mfupi baada ya kuapishwa. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya mambo atakayoyafanya mara baada ya kuapishwa:

Wahamiaji haramu mipakani

Ofisa Habari wa Trump, Karoline Leavitt aliwahi kunukuliwa na Fox News akisema: “tunajua aliahidi kutia saini agizo kuu la kulinda mpaka wa kusini.”

“Tunajua kwamba siku ya kwanza atazindua kampeni kubwa ya kuwarudisha makwao wahamiaji haramu wengi katika historia ya Marekani,” alisema.

Katika wiki ya kwanza baada kuchaguliwa tena, Trump ameweka kipaumbele katika kujaza nafasi za uongozi ambazo zingesimamia uhamiaji, na kupendekeza kuwa anajiandaa kushughulikia mipango yake ya sera ya mpaka mapema.

Alimgusa ofisa mkongwe wa uhamiaji, Tom Homan kama “mfalme wa mpaka”; alimchagua Gavana wa Dakota Kusini, Kristi Noem kusimamia usalama wa nchi; na kumteua Steven Miller kama Naibu Katibu Kiongozi anayeshughulikia sera katika Ikulu ya White House. Miller anafahamika zaidi kwa kutunga baadhi ya sera za Trump zinazoweka vikwazo zaidi kuhusu uhamiaji haramu katika muhula wake wa kwanza.

Mpango wowote wa kuwarejesha kwao watu wengi unaweza kukabiliwa na changamoto za vifaa pamoja na msururu wa changamoto za kisheria kutoka Uhamiaji na wanaharakati wa haki za binadamu.

Trump pia anaweza kutekeleza tena sera yake ya “Baki Mexico” ambayo inahitaji wanaotafuta hifadhi kusubiri hukohuko Mexico wakati maombi yao yanashughulikiwa.

Rais Joe Biden aliuita mpango huo kuwa “sio wa kibinadamu” na kujaribu kuumaliza katika siku yake ya kwanza ofisini, lakini alikabiliwa na changamoto za kisheria. Mwaka 2022, Mahakama ya Juu ilimruhusu kusonga mbele.

Wakati wa utawala wa Trump, takriban waomba hifadhi 70,000 walirudishwa Mexico kusubiri kusikilizwa kwao.

Ahadi nyingine ya siku ya kwanza ni kukomesha uraia wa kuzaliwa, kanuni ya miaka 150 ambayo inasema mtu yeyote aliyezaliwa katika ardhi ya Marekani ni raia wa Marekani.

Katika tukio la Januari 6, 2021, wafuasi wa Trump walivamia Bunge la Marekani (Capitol) wakati wabunge wakipiga kura ya kutokuwa na imani naye, wakishinikiza wabunge hao kuachana na mpango huo dhidi yake.

Baada ya kuchaguliwa tena, Trump hakutaja msamaha katika hotuba yake ya ushindi, lakini kwa muda mrefu alipendekeza kuwasamehe wale waliokutwa na hatia ya kuvamia jengo la Bunge (Capitol) mwaka 2021 itakuwa kipaumbele.

Alipoulizwa na Welker kwenye Meet the Press, Trump alisema “uwezekano mkubwa” angetoa msamaha.

“Nitafanya haraka sana,” alisema, akiita hukumu hiyo dhidi yao “siyo ya haki”.

Marais wa Marekani wana mamlaka makubwa ya kusamehe watu waliopatikana na hatia ya uhalifu au kumaliza vifungo vyao gerezani. Waendesha mashtaka pia wanaweza kuamua kufuta kesi zinazosubiri kutegemea ni nani Trump anaweza kuchagua kumsamehe.

Jambo lisilo wazi ni nani anaweza kupata msamaha huo.

Wakati mmoja, Trump aliiambia CNN: “Nina mwelekeo wa kuwasamehe wengi wao. Siwezi kusema kwa kila mmoja, kwa sababu wachache kati yao, labda walitoka nje ya udhibiti.”

Leavitt aliliambia gazeti la Washington Post kwamba ataamua “kwa msingi wa kesi kwa kesi atakaporudi White House.”

Zaidi ya watu 1,500 walikamatwa kuhusiana na ghasia za Capitol. Kulingana na namba za shirikisho, zaidi ya watu 750 kati yao walihukumiwa kwa uhalifu kuanzia kuingia bila ruhusa hadi kuwashambulia maofisa wa polisi na njama za uchochezi.

Licha ya kushinda uchaguzi wa mwaka jana, Trump pia amekabiliwa na changamoto za kisheria kufuatia uchaguzi wa mwaka 2020 na kesi tofauti ya nyaraka za siri.

Wakili maalum, Jack Smith, mwendesha mashtaka mkongwe aliyeteuliwa kusimamia uchunguzi wa Wizara ya Sheria ya Marekani kuhusu Trump, aliwasilisha mashtaka, ambayo Rais huyo mteule aliyakana.

Kulikuwa na taarifa kwamba Smith anapanga kujiuzulu kabla ya Trump kuchukua madaraka ili kuepuka ahadi ya Trump ya kumfuta kazi. Ripoti tofauti zilieleza kwamba ofisi yake itamaliza kesi mbili ilizokuwa ikifuatilia dhidi ya Trump.

Bado haijafahamika iwapo Trump na wafuasi wake watajaribu kumwadhibu Smith. Warepublican wa wabunge wameripotiwa kunuia kuchunguza kazi yake.

Kwenye kampeni zake, Trump alisema anaweza kumaliza vita nchini Ukraine “kwa siku moja”. Pia, mara kwa mara amekosoa uungaji mkono wa serikali ya Marekani kwa Ukraine, na hivyo kuvifanya vita hivyo kuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali.

Bado hajatoa maelezo maalumu jinsi atakavyojadiliana kuhusu kumalizika kwa vita hivyo zaidi ya kusema angesaidia nchi hizo mbili kufikia makubaliano.

Tangu kuchaguliwa kwake tena, Trump amezungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa njia ya simu ambayo ilidumu karibu nusu saa, huku bilionea Elon Musk, pia, akishiriki. Chanzo kimoja kiliiambia BBC kwamba “hayakuwa mazungumzo ya mambo muhimu sana.”

Ikulu ya Kremlin ilikanusha kuwa Trump alifanya mazungumzo na Vladimir Putin, ingawa ripoti za vyombo vya habari zilisema Trump alimuonya Rais wa Russia dhidi ya kuzidisha vita nchini Ukraine.

Uchumi ni suala ambalo Trump alilifanyia kampeni kubwa, akiapa kukomesha mfumuko wa bei mara tu atakapoingia madarakani.

“Tutalenga kila kitu kuanzia uwezo wa kumudu gharama za gari hadi uwezo wa kumudu kununua nyumba, gharama za bima hadi masuala ya ugavi,” alisema Trump kwenye kampeni zake.

“Nitalielekeza baraza langu la mawaziri kwamba ninatarajia matokeo ndani ya siku 100 za kwanza, au mapema zaidi kuliko hapo.”

Alisema atatia saini amri ya Rais ya utendaji ambayo inaelekeza kila waziri na mkuu wa taasisi “kutumia kila chombo na mamlaka waliyo nayo” kushinda mfumuko wa bei na kupunguza bei ya watumiaji.

Mpango wa Trump ni pamoja na kutoza kodi kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hasa zile zinazoingia kutoka China, akisema kodi hizo zitatengeneza ajira katika viwanda vya uzalishaji nchini Marekani.

“Mimi ni muumini mkubwa wa kodi. Nadhani kodi ndiyo neno zuri zaidi. Nadhani ni nzuri. Itatufanya kuwa matajiri,” alisema.

Trump ametetea sarafu ya mtandaoni, na ushindi wake uliifanya thamani ya Bitcoin kupanda kwa asilimia 30, kutokana na matarajio kwamba utawala wake utakuwa na sera rafiki zaidi.

Related Posts