CUF yajifungia kuandaa ilani ya uchaguzi, uteuzi wa katibu mkuu

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limejifungia kwenye kikao cha siku moja kujadili mambo mawili, ikiwemo kuandaa ilani ya uchaguzi ya Uchaguzi Mkuu 2025.

Pia, watatengeneza mikakati ya kudai Katiba mpya, lakini kupitia kikao hicho cha kwanza tangu kupata safu mpya ya viongozi wanatarajia kufanya uchaguzi wa baadhi ya watendaji wa chama hicho ikiwemo Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu aliyekuwapo alikuwa Hamad Masoud ambaye amemaliza muda wake na iwapo akiteuliwa anaweza kuendelea na majukumu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika funguzi wa kikao hicho, leo Jumatano, Januari 8, 2024, Mwenyekiti CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amewataka wajumbe wa Baraza hilo kujipanga na kuja na mipango yenye tija katika kujenga ilani hiyo ili ikawe mkombozi na kuleta ahueni ya kimaisha kwa wananchi wote.

“Lazima tuweke mkakati na kuja na sera ya kuhakikisha kila Mtanzania aweze kupata kipato kinacho mwezesha kujikimu kwa siku kwa kuanza na wazee ambao maisha yao kwa sasa ni magumu lazima tudumishe kama sera zetu zinavyotaka furaha kwa watu wate,” amesema.

Amesema shida wanazopitia wananchi lazima zipewe msukumo na wajumbe hao kwa kuwa wajumbe hao wanategemewa kuweza kusimamia haki na furaha kwa watu wote.

“Tuhakikishe rasilimali za nchi yetu zinatumika kwa manufaa ya Watanzania wote na inatubidi tuweke mkakati wa kuona nchi yetu inapata Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi na yenye misingi ya ujenzi imara,” amesema.

Profesa Lipumba amewataka wajumbe hao katika mapendekezo watakayotoa yaonyeshe dira nzuri ikiwa wanakwenda katika uchaguzi mkuu na chama hicho kikibahatika kuchaguliwa na wananchi kushika dola lazima lengo lao liwe kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

“Wajumbe wa Baraza Kuu mnakazi kubwa ya kufanya kuandaa mikakati katika kipindi hiki kifupi kuhakikisha kamati zetu zinaandaa sera na ilani ya uchaguzi kwa chama chetu kwa kutazama ilani zetu zilizopita na kuangalia michango iliyotolewa katika kuandaa dira ya Taifa ya mwaka 2050,” amesema.

Amesema iwapo ilani na mikakati yao itazingatia shida na matakwa ya wananchi watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuunganisha Watanzania wote na kuwaaminisha wanaouwezo wa kuwa mkombozi kwao.

“Tunahitaji kuandaa sera na ilani itakayokuja kufungua milango ya ajira kwa wananchi, uchumi shirikishi na kujenga demokrasia dhabiti ya kudumisha utawala bora,” amesema.

Awali, wakati Profesa Lipumba akikaribishwa kwenye kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, Othman Dunga amesema kwa mujibu wa Katiba yao kikao hicho kinafanya uamuzi wa chama.

“Kikao hiki kinawajumbe 50 lakini waliohudhuria katika kikao hiki ni wajumbe 44 kwa hiyo akidi ya kikao hiki imetimia na kitakuwa kikao halali na maamuzi yake yatakuwa halali vilevile,” amesema Dunga.

Related Posts