Njombe. Watumishi wa Afya katika Halmashauri ya Mji wa Njombe wametakiwa kuacha kuwatoza wagonjwa gharama yoyote kwa ajili ya usafiri wa gari la kubebea wagonjwa, kwani serikali tayari imeshagharamia huduma hiyo ili kuhakikisha wagonjwa wanapata usafiri wa bure.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 8, 2025 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Jabir Juma wakati wa hafla ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya Ihalula kilichopo Kata ya Utalingolo, Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Dk Juma amesisitiza kuwa hawatarajii kusikika malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kutozwa gharama za usafiri wa gari la wagonjwa, sababu lengo la serikali kutoa gari hilo ni kuboresha huduma za afya na kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za matibabu.
“Tusije tukasikia malalamiko kuhusu watumishi kuomba fedha za mafuta au gharama nyinginezo. Mwananchi ajue kuwa huduma hii ni bure,” amesema Dk Juma.
Amesema Halmashauri itaweka bajeti maalum kwa ajili ya matengenezo na mafuta ya gari hilo ili kuhakikisha linatoa huduma bila kusuasua.
Pia amewasihi wananchi kutumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan kwa wagonjwa walioko katika hali mbaya wanaohitaji huduma za dharura.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ihalula, Happiness Kwilasa amesema ujio wa gari hilo utapunguza changamoto za usafiri kwa wagonjwa, ambao mara nyingi wamelazimika kutumia gharama kubwa kufika hospitalini wanapohitaji rufaa.
Hata hivyo, Dk Kwilasa amebainisha changamoto nyingine zinazokikabili kituo hicho, ni upungufu wa watumishi na miundombinu duni, hasa nyumba za watumishi.
“Uhaba wa watumishi unapelekea kucheleweshwa kwa huduma muhimu kwa wagonjwa. Tunaomba serikali iangalie suala hili kwa karibu,” amesema Dk Kwilasa.
Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika amesema zaidi ya Sh2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, ikiwa ni jitihada za kuboresha huduma za afya.
“Tumefanikisha ujenzi wa vituo vitano vya afya, vinne kati ya hivyo vimejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, huku kituo cha Luponde kikiwa kinajengwa kupitia fedha za serikali kutoka kwenye tozo,” amesema Mwanyika.
Diwani wa Utalingolo, Erasto Mpete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, amewataka wananchi kuhakikisha gari hilo linatunzwa ili liwahudumie kwa muda mrefu.
“Magari haya yamekuwa yakitumika vibaya katika baadhi ya maeneo. Wananchi mnapoona matumizi yasiyo sahihi, toeni taarifa kwa mamlaka husika,” amesema Mpete.
Mkazi wa Kijiji cha Ihalula, Agnes Mbilinyi ameelezea furaha yake kuhusu ujio wa gari hilo, akisema limekuja wakati muafaka kwa sababu walikuwa wakipata changamoto kubwa hasa wakati wa usiku wanapokuwa na wagonjwa.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu. Gari hili litasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi,” amesema Mbilinyi.