Mwendokasi Mbagala bado kitendawili | Mwananchi

Dar es Salaam. Hatua ya kuitwa wazabuni wa kusambaza gesi asilia katika mabasi 755 yatakayotoa huduma katika awamu ya pili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), inatia moyo, lakini bado haitegui kitendawili cha lini awamu hiyo itaanza rasmi.

Jawabu la lini awamu hiyo itaanza kazi linabaki kuwa kitendawili kisichoteguka, kutokana na ahadi lukuki zilizowahi kutolewa bila utekelezaji kufanyika, hali inayowaacha wananchi bila matumaini.

Mei 20, 2023 Kaimu Meneja wa Mipango ya Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Mohamed Kuganda alisema awamu hiyo ya pili itakayohusisha mabasi zaidi ya 700 ingeanza kazi Desemba 2023.

Ahadi nyingine ilitolewa Agosti 2024 na Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia aliyesema awamu hiyo ya pili ingeanza rasmi Novemba 2024, baada ya kukamilika kwa mabasi yaliyokuwa yanatengenezwa.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala naye alitoa ahadi nyingine Agosti mwaka jana, akidai mabasi katika njia hiyo yangeanza huduma Desemba 2024, lakini ahadi zote hizo hazikutimia.

Juzi, Dart ilizialika kampuni mbalimbali za usambazaji wa gesi asilia kuomba zabuni ya usambazaji wa nishati hiyo kwa mabasi 755 yatakayotoa huduma awamu ya pili ya mradi huo.

Awamu ya pili ya Dart inahusisha huduma katika Barabara ya Kilwa  yenye urefu wa kilomita 20.3 na itatoka katikati ya jiji hadi Mbagala Rangitatu.

Kwa mujibu wa wito huo wa mzabuni, msambazaji huyo wa gesi atahusisha na usambazaji wa huduma hiyo kwa mtoa huduma wa mabasi, huku Dart ikiwa msimamizi wa shughuli zote.

Zabuni zote, kwa mujibu wa taarifa hiyo zinapaswa kuwasilishwa kabla ya Januari 29, mwaka huu.

Tangazo hilo la wito wa wazabuni, linafufua matumaini ya ujio wa mabasi hayo, tangu ilipotangazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wiki mbili zilizopita na amelisisitiza hilo hata alipozungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 8, 2025.

Msigwa amesema Serikali inatarajia kuleta mabasi 755 yatakayotoa huduma katika awamu ya pili ya mradi huo na yatatumia nishati ya gesi katika uendeshwaji wake.

Sambamba na mabasi hayo, Msigwa amesema mengine 177 yataletwa kwa ajili ya kuongezea idadi ya yanayotoa huduma katika njia za awamu ya kwanza ya mradi huo, yaani Barabara ya Morogoro.

Kwa mujibu wa Msigwa, mabasi yote yataletwa na sekta binafsi, ambayo Serikali imeamua kushirikiana nayo na hakuweka wazi majina ya kampuni hizo za sekta binafsi zitakazoleta usafiri huo.

Kuanza huduma kitendawili

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatato Januari 8 2025 baada ya kuulizwa lini itarajiwe mabasi hayo yataanza kutoa huduma, Dk Kihamia amesema taarifa yoyote kuhusu mwenendo wa huduma itatolewa pale wakala huo utakapoviita vyombo vya habari.

Lakini kwa sasa, amesema hana nafasi ya kulizungumzia hilo, kwa kuwa tayari kuna jambo linaloendelea, akimaanisha wito wa wazabuni kwa ajili ya usambazaji gesi.

“Hata hivyo, hapa nipo kwenye kikao. Lakini kwa jumla sipo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo na kama tutakuwa na lolote tutaviita vyombo vya habari na kuvieleza, lakini kwa sasa kinachoendelea ni hiyo taarifa ya zabuni,” amesema.

Dk Kihamia amesema kinachopaswa kuangaliwa ni tangazo la zabuni ya sasa ambalo maelezo yake yamejitosheleza.

“Tangazo hilo ni letu na maelezo yake yamejitosheleza, tujikite kwenye maelezo ya tangazo lililopo tusiulize ya nyuma wala mambo mengine,” amesema.

Akizungumzia historia ya mradi huo, mmoja wa wajumbe wa kamati iliyoundwa na Serikali mwaka 2002, kujadili na kujifunza juu ya uanzishaji wa mradi huo, Mujengi Gwao (sasa ni marehemu) alisema kamati hiyo ilihusisha wadau mbalimbali.

Wadau hao, alisema ni Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa) wakati huo kikiitwa Darboa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Gwao ambaye wakati huo, alikuwa Katibu wa Darboa, alisema kamati hiyo iliundwa mwaka 2002 na ilienda nchini Columbia, kujadili na kujifunza kuhusu uanzishaji wa BRT nchini.

Alisema kamati hiyo ilifanya mkutano wake wa mafunzo mjini Bogota, nchini Columbia mwaka huo, kisha kutoa mapendekezo mbalimbali ya namna ya utekelezaji wa mradi huo kwa Jiji la Dar es Salaam uliopangwa kutekelezwa kwa awamu sita.

Gwao, alisema kutokana na mahitaji ya huduma ya usafiri itakayoendana na idadi ya watu katika eneo hilo kwa makadirio ya mwaka huo, waliazimia mradi kwa jumla uwe na mabasi 2,000 na utekelezaji uanze mwaka 2005.

Related Posts