Samia: Maono ya Serikali kuzalisha wataalamu badala ya wasomi

Unguja. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema maono ya Serikali ni kusomesha watoto kuwa wataalamu wanaoweza kuajirika ndani ya miradi inayowekezwa nchini.

Amesema elimu inayotolewa inatakiwa kuzalisha wataalamu na si wasomi pekee, kwani mtu anaweza kuwa msomi lakini asiwe mtaalamu, hivyo kushindwa kujisaidia yeye mwenyewe na kushindwa kulisaidia taifa lake.

Rais Samia Suluhu Hassan afungua Skuli ya Sekondari Misufini, Bumbwini Zanzibar leo Januari 8, 2025 wakati wa shamrashamra za kuelekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Samia amesema hayo leo, Jumatano, Januari 8, 2025, wakati wa ufunguzi wa Shule ya Sekondari ya Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambayo ameiita jina la Makamu wa Pili mstaafu, Balozi Seif Ali Idd. Tukio hilo ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea Januari 12, 1964.

“Unaweza kuwa msomi lakini ulichokisomea kisikusaidie. Ila ukiwa mtaalamu wa eneo fulani, utakusaidia wewe, taifa, na jamii kwa ujumla. Lengo letu ni kutoa wataalamu watakaoweza kuajirika katika maeneo mbalimbali,” amesema Rais Samia.

“Kama mnavyoona, uwekezaji unaendelea nchini. Jana nilikuwa Bawe, ambako kuna hoteli ya kimataifa imewekezwa. Zimetoka ajira 400, lakini nilikuwa naangalia watu wanaofanana na sura za pwani (Wazanzibari). Kama wapo, ni wachache sana,” amesema.

Ameeleza hilo linaonyesha bado hawajafanikisha kazi ya kuzalisha wataalamu wa sekta ya utalii, hasa kutokana na changamoto za mila na desturi zilizokuwepo hapo awali. Wazazi hawakutaka watoto kufanya kazi hizo kwa sababu ya upotoshaji uliokuwepo kuwa ni kazi zisizofaa.

Rais Samia Suluhu Hassan afungua Skuli ya Sekondari Misufini, Bumbwini Zanzibar leo Januari 8, 2025 wakati wa shamrashamra za kuelekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hivyo, Rais Samia amewataka wazazi kuwaachia watoto kutumia fursa zilizopo, kwani wawekezaji wote wanaowekeza nchini wanazingatia vigezo vya kisasa, hivyo wanafunzi wanapaswa kupewa elimu inayooendana na soko la ajira.

Amehimiza wazazi kuwapa watoto muda mzuri wa kusoma, kwani huu ni wakati wao wa kujifunza ili kupata matokeo mazuri.

Sambamba na hayo, amewataka walimu kuboresha elimu kupitia kompyuta zilizopo ili kuongeza ufanisi kwao na kwa wanafunzi.

Akizungumza kuhusu mapinduzi, Rais Samia amesema kuna mabadiliko makubwa katika nyanja ya elimu. Mwaka 1964, kulikuwa na shule 62 tu, kati ya hizo sekondari tano na chekechea moja, zikiwa na wanafunzi 1,308.

“Ulikuwa ukitafuta shule za Zanzibar huzioni mbele kwenye ufaulu, ulikuwa unazikuta huko nyuma. Lakini sasa zinaonekana. Haya ni maendeleo makubwa,” amesema.

Ujenzi wa Shule ya Bumbwini

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said, amesema ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh6.1 bilioni na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,800

Shule hiyo ina madarasa, hosteli za wanafunzi wa kike na wa kiume, pamoja na nyumba mbili za walimu. Lengo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi wa eneo hilo.

Rais Samia Suluhu Hassan afungua Skuli ya Sekondari Misufini, Bumbwini Zanzibar leo Januari 8, 2025 wakati wa shamrashamra za kuelekea miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akitoa salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mattar Zahor Mohammed, amesema dhamira ya mapinduzi ni kuleta ukombozi wa kisiasa na kiuchumi, jambo linaloonekana kupitia miradi mikubwa ya elimu inayojengwa.

“Bila ya elimu, inawezekana tumejenga ukuta wa jiwe kwa watoto, kwa kuwafanya wasiweze kufikia fursa. Tunaona juhudi za kuuvunja ukuta huo ili watoto wetu waweze kuzifikia fursa zinazoendelea kuwepo,” amesema Zahor.

Aidha, amepongeza juhudi za Serikali tangu mapinduzi, akisisitiza kuwa maendeleo ya elimu ni sehemu muhimu ya ukombozi wa kijamii na kiuchumi.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa, amesema Serikali zote mbili zimewekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu ya elimu, maslahi ya walimu, vitendea kazi, na vifaa vya kisasa.

Mageuzi haya yamepelekea kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi, hatua inayothibitisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake.

Related Posts