Muya aibukia Geita Gold | Mwanaspoti

BAADA ya kutemwa na Fountain Gate, kocha Mohamed Muya ameibukia Geita Gold kuchukua mikoba ya Amani Josiah aliyetuaTanzania Prisons baada ya mwenyewe kuomba kuondoka ndani ya timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship.

Muya alitupiwa virago na Fountain Gate muda mfupi baada ya kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Yanga katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa mwishoni mwa mwaka jana kwenye Uwanja wa KMC Complex ambapo uongozi ulivunja benchi lililokuwa chini yake.

Chanzo cha kuaminika kutoka Geita Gold kimeliambia Mwanaspoti kuwa wamemalizana na kocha huyo ili aiongoze timu hiyo irudi Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Ni kweli mara baada ya kuachana na Josiah aliyeomba kuachia ngazi mwenyewe tumefanya mazungumzo na Muya na kufikia makubaliano sasa ndiye atakayekuwa kocha mkuu,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti lilimtafuta Muya ili azungumzie suala hilo, lakini alisema bado mchakato wa mazungumzo unaendelea na muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi.

“Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa, lakini kuna mazungumzo yanaendelea baina yangu na uongozi wa Geita Gold. Kama kila kitu kitaenda sawa taarifa itatolewa na viongozi na sio mimi,” alisema Muya.

Geita ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 14 ikikusanya pointi 30, imeachwa pointi tano na vinara wa ligi, Mtibwa Sugar yenye pointi 35.

Related Posts