MAAFANDE wa Tanzania Prisons wameongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kwa kumnasa mshambuliaji Kelvin Sabato ‘Kiduku’ aliyewahi kuwika na Mtibwa Sugar, Singida Big Stars na Namungo.
Usajili huu unakuwa wa kwanza kwa kocha mpya wa Prisons, Amani Josiah ambaye ana jukumu zito la kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika duru la pili la Ligi Kuu, kwani kwa sasa ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 14.
Akizungumzia uhamisho huo, Kiduku aligoma kuthibitisha kukamilika kwa dili hilo akisema anachoweza kuwahakikisha mashabiki wake ni kwamba wategemee kumuona Ligi Kuu Bara katika michezo iliyosalia ya duru la pili.
“Sio jukumu langu kusema nimesajiliwa na timu fulani, subirini wenyewe watatangaza. Nasubiri kwa hamu kurejea Ligi Kuu,” alisema.
Kocha Amani Josiah alisema: “Tunataka kufanya vizuri katika ng’we ya pili ya ligi, ni jambo ambalo linawezekana nani ataingia katika dirisha hili ni vizuri tukasubiri kwa sababu bado dirisha lipo wazi.”