Mama Mongella apaza kilio pensheni kiduchu kwa viongozi wastaafu

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kuangalia upya pensheni za wastaafu ili ziendane na za wastaafu wa sasa kwa kuwa wote mahitaji yao yanafanana na wote wanakabiliwa na mfumuko wa bei.

Wastaafu wa zamani wanatajwa kupokea malipo kidogo ya kila mwezi, jambo linalowafanya washindwe kumudu mahitaji yao ya kila siku kutokana na kupaa kwa gharama za maisha kunakoshuhudiwa miaka ya karibuni.

Hoja hiyo imeibuliwa na mwanaharakati wa haki za wanawake na mwanasiasa mkongwe nchini, Balozi Getrude Mongella katika mahojiano maalumu na Mwananchi, nyumbani kwake, Dar es Salaam hivi karibuni.

Maoni hayo ya Mongella yameungwa mkono na baadhi ya wastaafu pamoja na vyama vya wafanyakazi, ambaon pia wamependekeza malipo hayo yawe yanaongezwa kila mwaka kama ilivyo mishahara, ili kufanya kipato cha wastaafu kiendane na wakati.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amesema suala hilo limefanyiwa kazi na majibu yake yatatoka mwaka huu.

“Mama Mongella yuko sahihi, lakini hili ni suala la kisheria, hivyo tuliwapa mapendekezo wataalamu ambao walikaa kuangalia uwezo wa mfuko na kile unachotaka kulipa, wakipata majibu ndiyo watatufanya tuendelee,” amesema.

Baada ya wataalamu hao kufanya kazi na kukamilisha, mapendekezo yaliyotolewa yalipelekwa wizara inayosimmia mfuko ili iweze kupitia na ikitoa kibali ndio pensheni itaongezwa.

“Hivyo, linashughulikiwa. Kwa kweli kiwango cha chini tangu kuongezwa imekuwa muda mrefu, hivyo ndani ya mwaka huu tutakuwa na majibu sahihi ya kinachokwenda kufanyika, na si peke yetu,, hata wale upande wa Serikali wanaoshughulikia watumishi wa umma nako wanafanyia kazi hili,” amesema Mshomba.

Juhudi za kuupata uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Festo Fute amesema wamepokea mapendekeza kuhusu marekebisho ya pensheni na yanafanyiwa kazi na itakapoonekana hakuna tatizo watamshauri wizara husika.

“Tumeyapokea (mapendekezo) nadhani ya PSSSF na tunayafanyia kazi. Kwa sababu ni mchakato tutaangalia kama kuna hatari yoyote inaweza kutokea kwenye mfuko ikiwa pensheni hii itaongezeka, kama haitakuwepo tutamshauri waziri juu ya suala hili,” amesema.

Alipoulizwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema hoja ya Mama Mongella nii jambo la kisera linaloongozwa na sheria ya mwaka 2018 na iko chini ya kikokotoo maalumu kinachofanywa na mifuko husika.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema suala kwamba (wastaafu) walifanya kazi miaka mingi na wanalipwa fedha kidogo “linahitaji uamuzi tofauti na wa kipensheni na kiinchi.”

Amesema mahesabu ya pensheni yanatokana na hesabu zinazopigwa kutokana na michango ya mfanyakazi na kiwango cha mshahara; tofauti na hapo ni labda uamuzi mwingine utolewe, tofauti na ilivyo sera na sheria zinavyoelekeza.

Katika mahojiano hayo na Mwananchi, Mongella amesema wastaafu wa zamani wanapewa viwango vidogo vya pensheni ya kila mwezi ambavyo haviendani na wakati wa sasa ambao gharama za maisha zimepanda.

Kutokana na hilo, amependekeza pensheni wanayolipwa viongozi sasa hivi iwiane na viongozi wa zamani kwa kuwa kazi walizokuwa wanazifanya ni sawa, tena wao walikuwa kwenye mazingira magumu zaidi.

“Hapa namaanisha, kama mtu alikuwa ni waziri, basi alipwe mafao yanayofanana na waziri wa sasa. Kwa kuwa wote wanaishi maisha yaleyale ambayo bidhaa zimepanda bei.

“Lakini, pia, ikumbukwe hawa ndiyo waliochangia kuleta uhuru wa nchi hii na wao walikuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu zaidi, kwani nakumbuka ilifika mahali ukisafiri kwenda huko vijijini mwenyekiti wa mtaa anakupisha nyumba yake na wakati mwingine unakuta ina kunguni, lakini unalala hivyohivyo, utafanyaje uko kazini,” amesema.

Alipoulizwa kama anaona wastaafu wa enzi zao wanapewa thamani inayosthaili kupewa, amesema inategemea thamani ipi.

“Kama ni ya mali kwa kweli hatujapewa. Kwa sababu tukikwambia pensheni ambayo  tunaipata wapigania uhuru sisi, utasema masikini hawa watu. Hiyo kwa kweli sitaficha, hiyo thamani ya mali aaaah, au tuseme kitu cha kufuta machozi kwa kazi ambayo umeifanya haijalingana, mtafute mtu yoyote aliyeishi kipindi hicho cha nyuma,” amesema.

Mongella ambaye pia ni rais mstaafu huyo wa Bunge la Afrika amesema, “Ilifika mahali ukipata Sh100, 000 pensheni wewe ni mtu uliyekuwa mkubwa, kwa hiyo mimi nadhani viongozi walitizame.”

“Watu wananiona mtu, wananiheshimu napata shikamoo zangu kwa wingi, kwa kweli hilo sina tatizo nalo, isipokuwa hili la kusema huyu kwa thamani ya kazi aliyoifanya kwa nchi hii, kweli unampa Sh100,000 afanye nayo nini, kwa nini isilinganishwe ya kwamba nilistaafu nikiwa balozi au nilistaafu nikiwa waziri, basi na mimi nipewe anachopewa waziri sasa hivi anapostaafu tatizo liko wapi,” amehoji.

“Sababu hela ni zetu sote na sisi tusingeijenga nchi hii watu wanaopata mamilioni sasa hivi wangeyapata wapi. Kwa hiyo mimi silionei aibu, kwa haraka kabisa Serikali yetu na Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) najua ataweza kusikiliza hii,” amesema.

Walichokisema wastaafu wengine

Mmoja wa wastaafu, Raymond Tungaraza amesema kuna wastaafu waliokuwa kwenye taasisi za Serikali, pensheni zao ni chini ya Sh100, 000, huku akishauri iongezwe ili wamudu gharama za maisha.

“Nashauri angalau kila mwaka wawe wanaongeza asilimia kama ilivyo katika mishahara ya watu, walau hata asilimia 10 ndani ya miaka mitano kama yuko hai inaweza kuwa imeongezeka kidogo kwani kama alikuwa anapata Sh100, 000 basi itakuwa Sh150, 000,” amesema.

Amesema pensheni wanayopata watu wa zamani ni ndogo ikilinganishwa na zile wanazopata wastaafu wa sasa hivi.

“Kikokotoo cha zamani ulikuwa unapewa hela nyingi zinabaki kidogo, kwa kikokotoo kipya mtu aliyestaafu kama alikuwa akipata Sh100 milioni atapewa Sh35 milioni, mtu akistaafu anataka mali yake atumie anavyoweza, cha zamani unapata asilimia kubwa, ndogo ndiyo inabaki unapewa kidogokidogo,” amesema.

Mratibu wa Umoja wa Wastaafu Tanzania (REAT), Ezekiah Oluoch ameunga mkono hoja ya Mongella akisema ni mambo ambayo umoja huo umepambania muda mrefu bila ya mafanikio, licha ya kuwa sheria ya ongezeko la pensheni ipo pamoja na kanuni zake.

Akielezea undani, Oluoch amesema ni sheria ya pensheni ya kwa watumishi wa umma ya mwaka 2018 ambapo kanuni zake zilitungwa pia mwaka huohuo 2018 ikiwa na vipengele vikuu viwili.

“Moja ya vipengele, ni kima cha chini kisiwe chini ya asilimia 40 na mara ya mwisho kima cha chini kilichotangazwa na Serikali ilikuwa ni Sh345, 000.

“Kwa mshahara wa Sh345, 000 uliotangazwa mwaka 2023, huyu mtu pensheni yake ya mwezi atapaswa kulipwa si chini ya Sh156, 000 lakini si mifuko ya hifadhi ya jamii wala waziri, aliye tayari kutekeleza sheria.

“Hii yote ni kwa kuwa wastaafu hawathaminiwi na wanadharauliwa,” amesema Oluoch ambaye pia amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Oluoch amesema kipengele cha pili kilichopo katika sheria hiyo ni mfumuko wa bei utakapokuwa kuanzia asilimia moja hadi asilimia 10, nusu yake inaongezwa kwenye pensheni.

“Mwaka 2023 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 4.9, ambapo asilimia 50 ya 4.9 ni sawa na asilimia 2.45 kwa maana kila mwenye pensheni ndio kiasi cha asilimia anachopaswa kuongezewa, lakini hakuna anayejali licha ya sheria hiyo kuwepo,” amesema Oluoch.

Ameongeza pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo katika ngazi mbalimbali, wamekuwa wakionekana kama wasumbufu, huku akiwaonya walio kwenye mamlaka kuwa nao ni wastaafu watarajiwa na wanachofanya wao ni kuwatengenezea njia nzuri ya kustaafu.

Vilevile, Oluoch amesema wakati viongozi wa juu wakiwa wamejitengenezea sheria ya mafao mazuri, shida wanaiona zaidi kwa kada za Magereza, Polisi na Uhamiaji ambapo kuna mstaafu wa cheo cha sajenti anapokea pensheni ya Sh45, 000 kwa mwezi akisema ni uonevu wa hali ya juu.

“Pia tuliwahi kukutana na mkurugenzi wa maendeleo ya mkoa, ambaye cheo chake kwa sasa ni sawa na katibu tawala, huyu tulikuta analipwa Sh150,000, hii si sawa kabisa.

“Kwani wakati viongozi wetu wamejiwekea kulipwa pensheni ya asilimia 80 ya mshahara wa anayekuwepo madarakani, hebu ifikirie na hizi kada nyingine jamani, kwani hawa watu wana mchango mkubwa katika kuifikisha nchi hapa ilipo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema katika suala la kuongezwa kwa pensheni ya wastaafu, huenda Mongella akawa sawa, japokuwa asingependa kulizungumzia kwa kuwa wao wanafanya kazi na watu waliopo kazini kwa sasa.

Hata hivyo, katika kuhakikisha wafanyakazi wanakuja kuwa na pensheni bora, Nyamhokya amesema ndio maana wamekuwa wakipambana na vikokotoo na kupandishwa kwa mishahara, wakiamini watakapostaafu watakuwa katika maisha mazuri.

“Nisingependa sana kuzungumzia viongozi wastaafu kwa kuwa si watu tunaojishughulisha nao, lakini kwa wafanyakazi, sisi tumekuwa tukipambana kuhakikisha wanapata mishahara mizuri ambayo mwisho wa siku itazalisha mafao mazuri,” alisema Nyamhokya.

Akijadili suala hilo, mchambuzi wa masuala ya uchumi na jamii, Oscar Mkude amesema haoni kama kuna haja ya viongozi wastaafu kuongezewa pensheni badala yake ziangaliwe kada nyingine wakiwemo polisi na walimu, wauguzi ambao mishahara yao ni midogo na mafao yao pia ni madogo.

Akitoa sababu, Mkude amesema viongozi wanapokuwa kazini, wamekuwa na posho na marupurupu mengi ukilinganisha na kada zingine nyingi zikitokana na safari na vikao vya mara kwa mara.

“Kupitia posho na marupurupu hayo, anaamini kuna wengine hata mishahara yao wanaweza wasiiuguze mwaka mzima na zipo taarifa kuna ambao wanapokea kikao kimoja hadi Sh250, 000 sasa jiulize huyu kwa siku akihudhuria vikao vinne si ana mshahara wa mtu wa miezi miwili,” amesema.

Hata hivyo, amesema ni viongozi hawahawa katika maisha yao wameweza kusomesha watoto wao vizuri na wengine hadi nje ya nchi na kupata kazi bila kusumbuka, kwa kuwa wapo ndani ya mfumo.

“Haya tunayaona hata huko serikalini, watoto wa viongozi wanateuliwa katika nafasi mbalimbali ni kwa sababu waliweza kuwasomesha shule nzuri na wana vigezo na kupitia kazi nzuri walizonazo, wanaweza kuwatunza wazee wao kwa kiinua mgongo kidogo ambacho wamekuwa wakipata,” amesema.

Mchambuzi huyo, amesema endapo Serikali itakubali kuongezwa pensheni kwa wastaafu hao ni wazi inaenda kujiongezea mzigo mkubwa ambao hapo baadaye itashindwa kuubeba, ukizingatia moja ya watu wanaofilisi mifuko hiyo ni pamoja na viongozi wastaafu.

Related Posts