USHINDI ilioupata Kenya dhidi ya Kilimanjaro Stars na ule wa Burkina Faso mbele ya wenyeji Zanzibar Heroes, umeziweka timu hizo zilizoalikwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 katika nafasi mzuri ya kucheza fainali itakayopigwa Jumatatu ijayo, visiwani hapa.
Timu hizo mbili kila moja sasa ina pointi nne baada ya kucheza mechi mbili, huku Harambee Stars ya Kenya ikiongoza kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa mbele ya Burkina Faso, ilhali Zanzibar ikifuata na pointi tatu ilizonazo, wakati Kilimanjaro Stars ikiwa haina pointi wala bao.
Kilimanjaro Stars ilipoteza mechi ya pili mfululizo mbele ya Kenya juzi usiku kwa mabao 2-0, wakati Zanzibar ililala 1-0 na sasa kila timu imesaliwa na mechi moja, Kenya ikijiandaa kuvaana na wenyeji Zanzibar Heroes kesho Ijumaa, siku moja baada ya leo Burkina Faso kumalizana na Kilimanjaro Stars mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Gombani.
Matokeo yoyote mazuri iwe ya ushindi au sare dhidi ya wenyeji kwa kila moja yatawapeleka kubaki katika nafasi mbili za juu ambazo ndizo zinazotoa timu za kucheza fainali Januari 13.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ahmad Ally alisema licha ya timu kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili za awali, lakini haitakubali kupoteza tena leo mbele ya Burkina Faso hata kama haiendi fainali.
“Ni kweli tumekubali kufungwa na hatuna wa kumlaumu. Tumetumia wachezaji vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa nafasi ya kucheza. Tumeona tuwatumie wachezaji hao tofauti na wenzetu Kenya ambao wachezaji wao wengi ndio wataenda nao kwenye Chan,” alisema Ahmad, huku kocha wa Harambee, Francis Kimanzi akiongeza kuwa kiu yao ni kushinda kila mchezo ili kubeba taji la michuano hiyo.
“Baada ya kuanza kwa sare dhidi ya Burkina Faso, tulikaa chini na tujitafakari tumekosea wapi tukafanya maboresho kwa vile lengo letu ni kubeba ubingwa, tuliweza kurekebisha makosa na kupata ushindi dhidi ya Tanzania Bara na sasa tunamalizana na wenyeji Ijumaa ijayo (kesho),” alisema Kimanzi.