Wanaume 193 waugua kipindupindu Mbeya

Mbeya. Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, watu 261 wamebainika kuugua ugonjwa wa kipindupindu, kati yao wanaume ni 193, wakiwemo watoto 12 wenye umri chini ya miaka mitano.

Taarifa hizi zimetolewa na Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila, wakati wa kikao kazi cha kujadili mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.

Kikao hicho ambacho kilifunguliwa jana Januari 7, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa kikiwashirikisha maofisa afya, maendeleo ya jamii, madiwani, watendaji wa mitaa na kata, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, katika ukumbi wa Mkapa, jijini Mbeya.

Dk Mwasubila amesema licha ya wagonjwa 261 kutambuliwa na kupatiwa matibabu, bado kuna changamoto ya baadhi ya wagonjwa kujificha nyumbani, hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa huo. Kati ya kata 36 za Jiji la Mbeya, kata 10 hazijaripoti kesi za kipindupindu, huku kata ya Ilemi ikiwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa hao.

“Chanzo kikuu cha mlipuko huu ni matumizi ya maji machafu. Tumeweka mikakati ya pamoja ya kutoa elimu kwa jamii na kusisitiza utoaji wa taarifa za wagonjwa waliopo majumbani,” amesema Dk Mwasubila.

Aidha, amesema tayari kuna vituo vya kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu katika Hospitali ya Wilaya ya Igawilo, Kituo cha Afya Iganzo na Ndanyela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameagiza kila kata kuunda timu ya wataalamu wa afya watakaotoa elimu kwa kushirikisha makundi ya wananchi, viongozi wa dini na wazee wa mila.

“Wadau wote wa afya na mazingira mnapaswa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya mlipuko wa kipindupindu ili kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa haraka na kuokoa maisha ya wananchi,” amesema Malisa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sisimba, Jumapili Mwasenga ametaja kufumuka kwa chemba za maji taka kuwa moja ya visababishi vya mlipuko wa ugonjwa huo.

Amesena maji taga yanazagaa kwenye makazi ya watu na kuwa mazalia ya nzi wanaosambaza kipindupindu kwa haraka.

Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema shule zikifunguliwa ni marufuku wafanyabiashara kuuza vyakula, maji na juisi maeneo yote ya shule za msingi.

“Pia natoa maelekezo kwa wataalamu wa afya kufanya ukaguzi kwenye maeneo mbalimbali ili kuhakikisha hali ya usafi inazingatiwa hasa kwenye biashara za vyakula na vilabu vya pombe za kienyeji,” amesema Nchimbi.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Dk Salvatory Mhando naye amewataka watendaji wa mitaa kuelekeza nguvu zao katika ukaguzi wa vilabu vya pombe za kienyeji, akisema mazingira ya maeneo hayo yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi.

Mkazi wa Isanga, Salome Aloyce amesema mazingira duni ya vilabu vya pombe, pamoja na usafi hafifu wa baadhi ya mama lishe na wauzaji wa nyama choma, yanahatarisha afya za walaji.

“Serikali inapaswa kusitisha biashara hizi kwa muda hadi hali ya afya itakaporejea kuwa salama. Pia, wamiliki wa majengo wanapaswa kufanya maboresho, hususan kuwepo kwa vyoo bora,” amesema Salome.

Takwimu hizi zinahusu kipindi cha Desemba 2024 hadi Januari 6, 2025.

Related Posts