Reli ya Kaskazini kuboreshwa | Mwananchi

Arusha. Serikali imesema ipo mbioni kufanya maboresho makubwa ya reli ya Kanda ya Kaskazini kwa lengo la kupunguza msongamano wa malori ya mizigo yanayopita katika Jiji la Arusha kutokea Bandari ya Tanga.

Aidha imesema kumekuwa na msongamano mkubwa wa malori hayo yanayoelekea nchi jirani na kusababisha kero kubwa kwa watumiaji wa barabara.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Januari 8, 2025 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege Kanda ya Afrika(ACI),unaotarajiwa kufanyika Aprili 24 hadi 30, 2025 jijini Arusha.

Profesa Mbarawa amesema mbali na uboreshaji huo wa reli watajenga vituo vya kisasa vya makasha ya nchi kavu (ICD) ili kuhifadhia mizigo itakayoshushwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi mbalimbali.

“Serikali ilishatoa Sh420 bilioni kwa ajili ya kuboresha bandari ya Tanga ambayo kwa sasa imepiga hatua kubwa zaidi ya Bandari ya Mtwara. Ukishaboresha bandari lazima uboreshe miundombinu mingine,” amesema.

“Sasa reli ya Kaskazini ambayo inaanzia Dar es Salaam, Tanga hadi Arusha sisi tunaipa kipaumbele kikubwa, tunaenda kuiboresha ili bandari ifanye kazi kwa ubora unaostahili ,”amesema.

Kuhusu mkutano huo waziri huyo amesema utashirikisha washiriki wasiopungua 400 ambao lengo lake ni kuendeleza maslahi ya pamoja ya viwanja vya ndege, kukuza ubora wa kitaaluma na kusaidia maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa anga bara zima la Afrika.

Profesa Mbarawa amesema hadi Novemba 2024, ACI ina zaidi ya wanachama 75 wa viwanja vya ndege wanaoendesha zaidi ya viwanja vya ndege 265 katika nchi 54 pamoja na washirika 59 wa kibiashara.

“Mkutano huu utakuwa na faida mbalimbali kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ujuzi wazawa katika masuala ya usafiri wa anga na utalii kupitia kujifunza mbinu bora za kimataifa zinazotumika katika kuboresha sekta hizo,” amesema.

Akizungumzia Uwanja wa Ndege wa Arusha, waziri huyo amesema Serikali imeshatoa Sh11 bilioni kwa ajili ya kuweka taa kwenye uwanja huo ili uweze kufanya kazi kwa saa 24 na kuwa Mkandarasi ameshapatikana na uwekaji huo wa taa utatumia muda wa kati ya miezi nane hadi tisa.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema sekta ya uchukuzi ni muhimu kwenye kukuza na kuimarisha uchumi na utalii wa mkoa huo na kuwa kuboreshwa kwa reli kutapunguza msongamano wa malori ya mizigo pamoja na ajali zisizo za lazima ambapo kwa sasa malori yameongezeka kutoa 60 hadi 600.

“Tunashukuru Serikali kwa maboresho makubwa ya sekta ya usafirishaji ambapo tunaamini ndege zikitua saa 24 itakuza uchumi na utalii. Kuhusu maboresho ya reli itasaidia kupunguza ajali nyingi za barabarani,” amesema.

Related Posts