Watanzania 55, waliozamia Afrika Kusini, wapigwa faini ya Sh40,000 kila mmoja

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Watanzania 55  kulipa faini ya Sh40,000 au kwenda jela miezi sita kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kuondoka ndani ya Tanzania na kwenda Afrika Kusini bila kufuata taratibu za Uhamiaji.

Waliohukumiwa adhabu hiyo katika kesi ya jinai namba 574/2025  ni wafanyabiashara ambao ni James Mkadam (31), Shaban Bora (26), Hemed Jongole (25), Mathew Kazoka (45) na David Makota (29) ambaye ni Mhadisi wa Programu (Software engineer) pamoja na wenzao 50.

Hata hivyo washitakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kwenda kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 8, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Beda Nyaki, baada ya washtakiwa kukiri kosa lao na mahakakama kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Hakimu Nyaki amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa na wamekiri wenyewe shtaka lao, hivyo anawahukumu kila mshitakiwa kulipa faini Sh40,000 na wakishindwa kila mmoja atatumikia kifungo cha miezi sita gerezani.

Awali, akiwasomea hoja za awali, Wakili wa Serikali Hadija Masoud akishirikiana na Rafael Mpuya, alidai kuwa washtakiwa waliondoka nchini bila kufuata taratibu wa Uhamiaji wa kutoka na kuingia nchini.

Amedai washitakiwa hao walikwenda Afrika Kusini kinyume cha sheria.

Masoud amedai Desemba 31, 2024 washtakiwa hao walirudishwa kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kisha walipelekwa ofisi za uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa kwa njia ya maelezo.

Wakiwa ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa hao walikiri shtaka lao.

Pia leo, baada ya kuwasomea maelezo yao, washtakiwa wote walikiri shtaka lao linalowakabili ndipo walipotia hatiani na kuhukumiwa.

“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama iwape adhabu kali washtakiwa kwani kitendo walichofanya ni cha aibu kwa Taifa pia wameitia hasara Serikali kwa kugharamia safari kutoka Afrika Kusini na kuwaleta nchini,” amedai wakili Masoud na kuongeza.

“Fedha zilizotumika kuwagharamia washtakiwa hao kutoka Afrika Kusini na kuwarudisha ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zingeweza kutumika katika miradi ya maendeleo na afya,” ameongeza Wakili Masoud.

Kwa upande wa washtakiwa, wao waliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni kosa lao la kwanza na hawatarudia tena, huku wengine wakiomba waachiwe huru na mahakamani hiyo bila kupewa adhabu.

Hata hivyo Hakimu Nyaki ametupilia mbali ombi la washtakiwa hao la kuwapunguzia adhabu na badala yake amewahukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh40,000 au kwenda jela miezi sita, kila mmoja.

Washtakiwa baada ya kupewa adhabu hiyo, walisimama na kumshukuru Hakimu kwa kuwapa adhabu hiyo kwa kukunja mikono na kuweka kifuani na kisha kuinamisha vichwa chini wakiashiria kuwa wanashukuru kwa adhabu hiyo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 31, 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), uliopo wilaya ya Ilala.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walikuwa wametoka isivyo halali katika ardhi ya Tanzania bila kibali na kueleleka Afrika Kusini.

Related Posts

en English sw Swahili