Afariki dunia akidaiwa kunywa pombe za kienyeji

Babati. Mkazi wa Mtaa wa Sawe, Kata ya Maisaka, mjini Babati mkoani Manyara, Yona Angres amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa ni kunywa pombe nyingi za kienyeji kupita kiasi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 8 mwaka 2025 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Makarani amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho cha mkazi huyo wa Mtaa wa Sawe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sawe, John Paul amesema Angres amefariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi za kienyeji kupita kiasi.

“Baadhi ya watu waliokuwa nao kwenye eneo hilo, wameeleza kuwa Angres alikunywa pombe nyingi za kienyeji na kufariki dunia,” amesema Paul.

Mkazi wa Mtaa wa Sawe, Isack Dere ameitaka jamii ya eneo hilo kunywa pombe zilizopitishwa na mamlaka husika kuliko kunywa pombe za kienyeji.

“Hapa Babati kuna kiwanda kizuri cha vinywaji changamfu, sasa kwa nini mtu unakunywa mataputapu hadi ufariki dunia kabla ya muda wako,” amesema Dere.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Asia Juma amesema Angres ni kijana aliyekuwa anafanya vibarua mbalimbali ikiwemo kubeba maji na kulipwa fedha.

“Nadhani siku hiyo hakula chakula ndiyo sababu akafariki dunia kwa kunywa pombe nyingi za kienyeji kupita kiasi,” amesema.

Related Posts