Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema Serikali inapaswa kuanzisha mifumo rahisi ya mikopo kwa wananchi ili kuwarahisishia kuepuka mikopo isiyo rasmi maarufu kama mikopo umiza au kausha damu inayowaletea changamoto.
Chama hicho kimesema aina hiyo ya mikopo inayotolewa na taasisi zisizo rasmi, imekuwa changamoto kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini.
Hata hivyo, ikumbukwe Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshazionya mara kadhaa taasisi zinazotoa mikopo bila ya kuwa na leseni, huku ikisema adhabu kwa watakaobainika ni faini ya Sh20 milioni au kifungo cha miaka miwili jela, au vyote kwa pamoja.
“Pia, kifungu cha 16(2) (a) cha sheria hiyo kimeainisha adhabu inayopaswa kutolewa kwa kuendesha biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili, au vyote viwili kwa pamoja,” ilieleza taarifa ya BoT iliyotolewa hivi karibuni.
Akizungumza leo Jumatano Januari 8, 2025, makao makuu ya chama hicho Magomeni Jijini Dar es Salaam, waziri mkuu kivuli wa ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita amesema mwaka 2024 Watanzania wengi wameteswa na mikopo umiza na ile ya kausha damu kwa kulipishwa riba kubwa isiyolingana na hali yao ya kiuchumi.
“Kwa mfano, mwaka 2024 pekee, ripoti zinaonyesha zaidi ya asilimia 30 ya wakopaji walishindwa kulipa mikopo yao, hali iliyosababisha kupoteza mali zao za thamani kama ardhi na nyumba,” amesema Mchinjita.
Amesema uhaba wa sera thabiti za kusimamia mikopo na uangalizi mdogo wa taasisi zinazotoa mikopo, umesababisha ongezeko la mikopo holela ambayo kwa sehemu kubwa imechochewa na kutodhibitiwa kwa sekta hiyo.
Amesema kukosekana kwa uanzishwaji wa mifumo rahisi ya mikopo kwa wananchi, nayo ni sababu iliyowafanya wakopaji kukimbilia kwenye mikopo ya masharti magumu.
“Kukosekana kwa mifumo salama ya mikopo kunawafanya wananchi kukosa fursa za kiuchumi, huku taasisi za kifedha zikiendelea kunufaika kwa kuwanyonya wananchi,” amesema waziri huyo kivuli.
Hata hivyo, kupitia taarifa ya Benki Kuu iliyotolewa Desemba 31, 2024, imewataka wananchi kutokopa kwa taasisi zisizo na leseni.
Kwa mujibu wa kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi, kampuni na watu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
Kutokana na hilo, BoT inasisitiza umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni.
Katika upande wa ajira, Mchinjita amesema mwaka 2024 haujatoa nafuu ya ugumu wa maisha, huku kundi la vijana limeendelea kukosa ajira na shughuli za kueleweka za kujiingizia kipato, huku akiishauri Serikali kuajiri zaidi.
Katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na mikopo holela iliyopewa majina tofauti kama mikopo umiza, kausha damu, mikopo ya nyoka na kobe inayotolewa na kampuni au watu binafsi wasio na leseni halali za Benki Kuu.
Mikopo hiyo inatajwa kuwa na riba kubwa pamoja na kero hata kufilisi mali za wakopaji pale wanaposhindwa kurejesha kwa wakati, huku masharti yakihusisha muda mfupi wa urejeshaji, jambo ambalo linafanya wengi washindwe kutimiza masharti ya mikopo hiyo.