Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF), kimemfuta uanachama mbunge wake wa Mtambile visiwani Pemba, Seif Salim Seif kwa kile kilichodaiwa amekisaliti chama hicho na kukiunga mkono chama tawala cha CCM.
Hatua ya Seif kufukuzwa uanachama, inamuondolea uhalali wa kuwa mbunge, hivyo wananchi wa Mtambile watakosa mwakilishi hadi hapo Uchaguzi Mkuu utakapofanyika baadaye Oktoba 2025.
Seif ameponzwa na kauli yake aliyoitoa hadharani wiki iliyopita, akiunga mkono juhudi za Serikali ya CCM chini ya Rais Hussein Mwinyi visiwani Zanzibar na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Tanzania kwa jumla.
Katika kauli yake hiyo, Seif alisema kuwa mwenendo wa utendaji wa Dk Mwinyi na Rais Samia, ana uhakika kwamba CCM itashinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Uamuzi wa kufukuzwa kwa Seif, umetolewa leo Jumatano, Januari 8, 2025 na Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kilichofanyika katika ofisi ya Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika ndani ya baraza hilo, uamuzi huo umefikiwa kutokana na kauli ya Seif kuwa, ana uhakika CCM itashinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Chanzo hicho kinasema, kitendo hicho cha Seif ni kukisaliti chama hicho, kukikosea heshima na kujenga taswira kwamba wananchi hawapaswi kukiamini.
“Kwa kauli yake, ni kwamba amefanya mazingira yoyote ya kukihujumu chama ili CCM ishinde kwenye uchaguzi ujao,” kinaeleza chanzo hicho.
Mwananchi ilimtafutwa mwanasheria wa chama hicho, Mashaka Ngole alikiri kuwepo kwa hilo, huku akifafanua jukumu alilopewa ni kuandika barua kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Spika wa Bunge kumtaarifu kuhusu uamuzi huo.
“Tutamtumia barua Spika wa Bunge na nadhani ndani ya wiki hii tutakuwa tumekamilisha itategemea na tutakavyoiharakisha, lakini mapema itakuwa imemfikia,” amesema Ngole ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Mwanasheria huyo amesema katika Kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya ameshinda kwa kupata kura 29 za ndiyo, huku Ali Juma Hamisi akishinda Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kwa kura 41 za ndio kati ya kura 45.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, CUF ilipata viti vitatu vya ubunge wa majimbo ya Mtwara Vijijini (Shamsia Mtamba), Pandani (Maryam Said) na Mtambile (Seif Salim Seif).
Mwananchi ilipomtafuta Seif, amesema hajapokea taarifa ya kufukuzwa uanachama hadi muda anaozungumza na Mwananchi saa 9:10 alasiri.
Kwa sababu hiyo, alieleza inakuwa vigumu kuzungumza zaidi, kwani hana historia ya migogoro na chama chake tangu alipojiunga na hata kuwa mbunge.
“Tangu nimekuwa mwanachama wa CUF, sikuwahi kuwa na mgogoro na chama changu na sikumbuki kama nimewahi kuitwa na kamati ya maadili, kwa hiyo mimi bado ni mwanachama halali,” amesema Seif.
Hata hivyo, amekiri kueleza mwelekeo wa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akifafanua imetokana na kazi iliyofanywa na viongozi wa chama hicho visiwani humo.
Amesema haoni dhambi kwa mwanasiasa kusema kiongozi fulani kwa utendaji na uwezo wake, anaweza kushinda uchaguzi unaokuja au uliopo.
“Mimi nipo Unguja na Pemba nimeona utendaji wa Dk Mwinyi ni mkubwa na wananchi wengi sasa hivi wanatazama nani analeta maendeleo sio propaganda.
“Na maoni ya wananchi wa Pemba wanaunga mkono juhudi za Dk Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan na baada ya kugundua hilo nikasema mwelekeo unaonekana viongozi hawa wana asilimia kubwa ya kushinda, kosa liko wapi,” amesema Seif.
Mwaka 2017, CUF iliwahi kuwafukuza wabunge wake wanane wa viti maalumu ambao ni Halima Ali Mohamed, Khadija Ally, Salma Mwassa, Miza Haji, Raisa Mussa, Riziki Mngwali, Saumu Sakala na Severina Mwijage. Mwingine aliyewahi kufukuzwa ni Hamad Rashid.
Sakata la wabunge kufukuzwa uanachama liliwahi kutokea hata kwa CCM, ilipomfukuza Sophia Simba mwaka 2017.
Kadhalika Chadema iliwahi kufanywa hivyo na, ilipomfukuza Zitto Kabwe na wabunge 19 wa viti maalumu akiwamo Halima Mdee na suala hilo lilienda mahakamani.