Ujenzi daraja lililovunjika Same wafikia asilimia 95

Moshi. Ujenzi wa Daraja la Mpirani lililovunjika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara katika Barabara Kuu ya Same-Mkomazi, Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro umefikia asilimia 95.

Daraja hilo ambalo lipo Kata ya Maore lilivunjika Januari 2, 2025 mwaka huu baada ya nguzo zilizokuwa zimelishikilia kuathiriwa na mafuriko kufuatia mvua zilizonyesha Desemba 20, 2024.

Kuvunjika kwa daraja hilo, ambalo ndio kiungo cha kata na makazi ya wananchi wanaoishi katika safu za milima ya Upare ilisababisha adha kubwa ya usafiri kwa wananchi hao.

Januari 4, 2025 mwaka huu, Waziri wa ujenzi, Abdallah Ulega alipita na kukagua ujenzi wa daraja hilo ambapo aliagiza Tanroads kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika ndani ya siku tatu na hadi kufikia leo Januari 8  liwe limepitika.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 8, 2025, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema ujenzi huo unakwenda vizuri na kufikia kesho Januari 9, 2025 asubuhi litaanza kupitika.

“Kazi inakwenda vizuri na kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 95 na kufikia kesho asubuhi, tunatarajia magari yataanza kupita,” amesema Kyando.

Akizungumzia daraja hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kujenga daraja hilo na kurejesha mawasiliano katika  barabara hiyo kufuatia ujenzi unaoendelea.

“Zoezi la kurejesha mawasiliano ya barabara inayounganisha kata za Ndungu na Maore linaendelea, lipo katika hatua za mwisho,” amesema Mgeni.

Amewaomba wananchi na watumiaji wa barabara waendelee kuwa watulivu wakati kazi ya kurejesha mawasiliano ikiendelea na waendelee kuchukua tahadhari wakati wote wanapoona kuna dalili za mvua kubwa ili kuepusha majanga.

Diwani wa Maore, Rashid Juma amepongeza jitihada zinazofanywa na Tanroad kurejesha mawasiliano katika eneo hilo ili kurudisha shughuli za kuchumi katika eneo hilo.

“Daraja hili ni kiungo muhimu sana kwa wananchi wa milimani na mpaka sasa tunaona kazi inakwenda vizuri na tunatarajia mpaka kufikia kesho kazi hii inaweza kuwa imekamilika na mawasiliano yatarudi kama kawaida,” amesema Juma.

Related Posts