DKT NCHEMBA AWAALIKA WAWEKEZAJI KUTOKA JAPAN

Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa wito kwa Kampuni za Japan kuwekeza nchini Tanzania ili kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uzalishaji kwa faida ya pande zote mbili.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma wakati akiagana na Balozi wa Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe.Yasushi Misawa, ambapo pamoja na mambo mengine, alimhakikishia pia Balozi huyo kuwa Tanzania na Japan zitaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kijamii kwa faida ya nchi hizo mbili.

Alisisitiza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo sekta ya kilimo itakayoiwezesha Tanzania kuwa ghala la chakula lakini pia uwekezaji katika miundombinu ikiwemo uendeshaji wa Reli ya Kisasa SGR.

Aidha, katika mazungumzo yao, Dkt. Nchemba aliishukuru Japan kwa uwekezaji mkubwa uliochangia maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na nchi hiyo katika sekta za kilimo, afya, nishati, na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Barabara ya mzunguko katika jiji la Dodoma.

“Katika kipindi chako pekee, tumeshuhudia Tanzania na Japan zikisaini mikataba ya mikopo nafuu yenye thamani ya yen ya Japan bilioni 10 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 151 pamoja na msaada wa yen bilioni 5.5, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 83. Tunakushukuru sana na tunakuomba uendelee kuwa Balozi mzuri wa Tanzania hata baada ya kumaliza muda wako” Alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Yasushi Misawa, aliyeambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Ara Hitoshi, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na nchi yake umedumu kwa zaidi ya miaka 60 ambapo katika kipindi hicho, Japan imesaidia utekelezaji wa zaidi ya miradi 360 ya kijamii na kiuchumi.

Alibainisha kuwa baadhi ya miradi hiyo iko katika sekta ya nishati ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga, ujenzi wa mradi wa umeme unaounganisha Tanzania na Kenya pamoja na mpango unaoendelea kati ya Tanzania na Japan kupitia Wizara ya Nishati wa kujenga mradi wa umeme wa joto ardhi.

Katika mazungumzo yao ambayo yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, viongozi hao walijadili fursa mbalimbali za maendeleo katika sekta za kilimo, afya, miundombinu, na kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Related Posts