Kocha Bravos: Simba? Tatizo ni Ahoua

KIKOSI cha Simba kimeondoka alfajiri ya leo kwenda Angola kuwahi pambano la raundi ya tano la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis, huku kocha wa wenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Jumapili akifichua Wekundu hao wamewatia ubaridi kwa namba walizonazo, lakini wakitishwa zaidi na nyota mmoja matata.

Simba iliyopo nafasi ya pili katika Kundi A linaloongozwa na CS Constantine ya Algeria itakuwa wageni wa Bravos yenye pointi sita inayoshika nafasi ya tatu baada ya awali kuifunga bao 1-0 Dar es Salaam, na ushindi utambeba Mnyama kwenda robo fainali kabla ya mechi ya mwisho dhidi ya timu ya Algeria.

Wakati Simba ikiondoka alfajiri ya leo kwenda Luanda, kocha wa Bravos, Mario Soares amekiri anatarajia mchezo mgumu dhidi ya wawakilishi hao wa Tanzania, huku akiweka wazi nyota anayemhofia zaidi ni kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua.

Timu hizo zitakutana Jumapili  kwenye Uwanja wa Taifa wa Novemba 11 (Estadio Nacional 11 de Novembro) uliopo Talatona jirani na Jiji la Luanda, huku kocha huyo akisema anatishwa na Ahoua aliyewatungua bao la penalti Kwa Mkapa kutokana na namba alizonazo na hatari aliyonayo mbele ya wapinzani.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Angola, Mario alisema Ahoua ni mchezaji mzuri kutokana na kiwango chake japo anaamini Simba kiujumla imeimarika zaidi tofauti na mchezo wa kwanza waliokutana Kwa Mkapa, anajua kabisa Jumapili hakutakuwa na mechi nyepesi kwa pande zote kutokana na umuhimu wake.

“Nafikiri ni mchezo unaoweza kutoa taswira kwa timu zote mbili katika harakati za kufuzu hatua inayofuata. Ahoua ni mchezaji mzuri aliyeleta mabadiliko chanya, lakini tutapambana pia kuhakikisha tunapata ushindi nyumbani,” alisema Soares.

Kocha huyo aliongeza licha ya kupoteza mchezo wa mwisho kwa kuchapwa mabao 4-0 ugenini mbele ya CS Constantine, lakini amekaa na wachezaji na kuwataka kusahau kilichotokea ili wawekeze nguvu katika mechi ijayo itakayotoa taswira kwao, hususan kutafuta mbinu za kuwadhibiti nyota wa Simba akiwamo Ahoua aliyedai ni tatizo.

Kauli ya Soares inadhihirisha ubora wa Ahoua ambapo katika michuano ya kimataifa hadi sasa hatua ya makundi amefunga mabao mawili sawa na Kibu Denis, huku moja likifungwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, lakini akiwa na asisti mbili ikiwamo aliyomsetia Kibu walipoichapa Sfaxien na ile ya Tshabalala walipolala ugenini mbele ya Constantine.

Moto wa nyota huyo sio katika michuano ya kimataifa pekee tu kwani hata kwenye Ligi Kuu Bara amechangia jumla ya mabao 12 kati ya 31 yaliyofungwa timu nzima msimu huu, akifunga mwenyewe saba na asisti tano.

Wakati Soares akianza kuingiwa na mchecheto, kikosi cha Simba kimeondoka leo kwenda Angola kwa ajili ya mchezo huo, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akiwataka wachezaji kwenda kuonyesha nidhamu kama walivyofanya ugenini na CS Sfaxien.

“Hatujapata muda mrefu wa kupumzika lakini bado tunaendelea kuishi katika malengo tuliyojiwekea, umuhimu wa mchezo wa Jumapili sio kwetu pekee, bali hata kwa wapinzani. Tutapambana ili kushinda na kupunguza presha ya mechi ya mwisho,” alisema Fadlu.

Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 40, baada ya kucheza 15 imeshinda 13, sare moja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao 31 na kuruhusu matano, ikiwa na wastani mzuri tofauti na wapinzani wao katika kundi lake.

Kwa upande wa Bravos katika Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’ imecheza pia michezo 15 ambapo imeshinda minne tu, sare minane na kupoteza mitatu, ikiwa nafasi ya tano na pointi 20, nyuma ya vinara Petro Atletico yenye pointi 33.

Katika michezo hiyo kikosi hicho kimefunga mabao 14 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12, jambo linaloonyesha wazi hakipo vizuri katika maeneo mawili ya ushambuliaji na uzuiaji, kitu kinachoweza kuipa faida Simba itakapokutana nayo.

Hata hivyo, katika michezo minne ya nyumbani ikiwemo miwili ya raundi ya awali na miwili ya makundi, Bravos haijapoteza mchezo wowote, kwa sababu kati ya hiyo imeshinda mitatu kwa mabao matatu, huku mmoja tu pekee ikishinda kwa bao 1-0. Bravos iliichapa Coastal Union hatua ya awali ikiwa nyumbani mabao 3-0, na kutoka suluhu jijini Dar es  Salaam na kufuzu kwa jumla ya mabao 3-0, kisha kuitoa pia FC Lupopo ya DR Congo, ambapo nyumbani ilishinda 1-0 na ugenini kushinda 2-1.

Katika hatua hii ya makundi, Bravos ilizichapa CS Constantine ya Algeria na Sfaxien ya Tunisia kila moja kwa mabao 3-2, na sasa inacheza na Simba, ikiwa ni mchezo ambao utatoa taswira nzima kwao ya kutinga robo fainali ya Shirikisho Afrika.

Related Posts