WAKATI mabosi wa Yanga wakiwa mezani kumalizana na mshambuliaji anayemudu kucheza kama winga, Jonathan Ikangalombo, kocha wa zamani wa AS Vita anayotoka nyota huyo wa DR Congo, amefunguka juu ya makali ya mchezaji huyo akisema mabingwa wa Tanzania wamepata mtu wa kutengeneza mabao na kufunga.
Kocha Raoul Shungu, aliyewahi kuzinoa Yanga na AS Vita kwa vipindi tofauti, alisema kama dili la nyota huyo litatiki Jangwani, basi timu yake hiyo ya zamani itakuwa imepata mtu wa maana mwenye uwezo wa kuisaidia kwani Jonathan ana pua ya kunusa nyavu na kusaidia wengine kutupia
Shungu alisema Jonathan ni winga asili wa kulia ambaye anajua kutengeneza nafasi za mabao akiwa na kasi na akili ya kuwapenya mabeki wa timu pinzani, mbali na kutengeneza nafasi pia ana uwezo wa kufunga, ambapo akiwa Vita alitengeneza safu bora ya ushambuliaji akisaidiana na Elie Mpanzu kabla naye hajatimkia Simba.
“Ikangalombo (Jonathan) ni winga mzuri anajua sana kutengeneza nafasi. Huyu anafaa kushambulia akitokea pembeni kulia au hata kushoto itategemea kocha wake atatakaje,” alisema Shungu aliyewahi kuiongoza Yanga katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998.
“Namjua Ikangalombo tangu akiwa Motema Pembe kabla ya kutua AS Vita, kwanza Yanga kama itampata imepata mchezaji mwenye adabu anayejua kutafuta maisha, sijawahi kuona akifanya mambo ya hovyo,” alisema Shungu na kuongeza:
“Kitu kingine anajua pia kufunga, anajua kupunguza mabeki na kutengeneza nafasi mabeki wa timu pinzani watatakiwa kumchunga sana, akimudu pia kucheza kama mshambuliaji.”
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha kuwa, Jonathan katika mechi 12 ambazo AS Vita inaongoza kundi la Ligi Kuu DR Congo, ametumika mechi sita, huku akikosa sita vilevile na amefunga bao moja na kuasisti mara mbili.
Shungu aliwatoa hofu mashabiki wa Yanga akisema licha ya winga huyo kutocheza mechi nyingi, lakini bado ana imani atakuwa na maisha mazuri ndani ya soka la Tanzania.
Shungu aliongeza, Yanga ya sasa haina winga asili kwenye kikosi chake na kwamba, Jonathan atakuwa mtu sahihi endapo kocha atahitaji kuwa na mtu mzuri atakayeshambulia kutokea pembeni.
“Hiyo kutocheza mechi sita sioni kama ni tatizo sana. Jambo zuri yupo sawa sasa kucheza, nadhani atafanya vizuri hapo Tanzania, ligi ya hapo naijua. Uzuri wake ni mtu mwenye nguvu anajua kupambana na mabeki. Bahati nzuri ni kwamba Yanga haina winga halisi, zaidi naona inawatumia viungo washambuliaji katika nafasi hizo. Huyu atawafaa sana kama watamalizana na kuanza kumtumia,” alisema.
Mchezo wa mwisho kwa Jonathan kuichezea AS Vita ulikuwa Novemba 24, mwaka jana katika dabi dhidi ya Renaissance akifunga bao pekee lililoipa ushindi timu hiyo akiibuka nyota wa mchezo.