WAKAZI WA SAME WATAKIWA KUENZI MABADILIKO YA MIUNDOMBINU NA UCHUMI YANAYOWEKEZWA NA SERIKALI

Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wananchi wa wilaya ya Same kutambua na kumiliki mafanikio ya serikali kwa kutunza na kulinda miundimbinu inayowekezwa kwenye maeneo yao pamoja na kujenga tabia ya kuenzi mabadiliko makubwa ya miundombinu ya huduma na uchumi ambayo imewekezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa elimu kwa wananchi wenye utambuzi mdogo, wanaopinga maendeleo ili iweze kuwasaidiwa katika uelewa juu ya juhudi za serikali katika uwekezaji wa miundombinu yenye gharama nyingi.

Akizungumza na wakazi wa kata ya Suji wilayani Same, mara baada ya ziara ya kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi miwili ambayo ni mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Suji pamoja na Zahanati ya Malindi – Suji ambapo amesema uwekezaji huo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Afya ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Malindi kata ya Suji ambayo inaelezwa kuwa awali wakazi wa kata hiyo walilazimika kutembea umbali wa kilomita kumi (10) kutafuta huduma za Afya, Mradi huo ambao uliibuliwa na wananchi unatekelezwa na Jamii, Halmashauri ya wilaya ya Same pamoja na Ubalozi wa Japani upo hatua za mwisho kukamilika huku gharama zake zikiwa ni milioni 470 hadi sasa.

Kutokana na uhitaji wa huduma zaidi za kiafya katika eneo hilo Waziri wa Afya ameahidi kupandisha zahanati hiyo na kuwa Kituo cha Afya ili huduma zote muhimu ziweze kutolewa lengo ikiwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Kwa umbali huu na milima hii, Tusipoimarisha zahanati yetu, vyumba vya kujifungua na huduma za upasuaji tutakuwa bado tuna changamoto, Tunalo jukumu la kupunguza vifo vya akina mama wanaojifungua, Tunaleta fedha hapa milioni 600 kupandisha hadhi zahanati hii kwa mwaka wa fedha 2024/25 ili majengo yote yajengwe hapa tuokoe vifo vya mama na mtoto, Haya ndio maono ya Rais Samia kwa wananchi” Amesema Waziri Mhagama.

Hali ya jiografia ya eneo hili ni milima na mabonde, kutokana na hali hiyo Waziri Mhagama ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Same kuhakikisha maeneo yenye miradi yanawekewa mazingira mazuri kwa kuchonga miinuko ambayo inaweza kuathiri miundombinu wakati wa mvua na kusababisha majanga kwa watumiaji wa miundombinu hiyo hasa shule.

“Ardhi yetu ina milima, na huwezi kutoa jingo bora bila kuchonga milima gharama imekuwa kubwa, hakika kunahitajika serikali na halmashauri (Same) tuhakikishe hii milima inatengenezewa uzio iimarike isije ikaporomoka na kuingia kwenye madarasa ya watoto wetu, Nikuagize Mkurugenzi, kupitia bajeti ya ndani wekeni bajeti ili kuweka sawa miundombinu hii ili shule yetu iwe salama na idumu kwa muda mrefu” Amesema Waziri Mhagama.

Awali mkuu wa wilaya ya Same amesema kuwa miradi hii itaendelea kutunzwa na kusimamiwa ipasavyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kama iliyokusudiwa.

Related Posts