Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amewaonya wananchi waliotaka kumshambulia mwananchi mmoja wakimtuhumu kuwa ni mbakaji maarufu ‘Teleza’.
Kamanda Mutafungwa ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 9, 2025 katika taarifa kwa umma iliyochapishwa katika kurasa za mitandao ya kijamii ya Jeshi la Polisi.
“Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linapenda kuwatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususan wakazi wa kata ya Mkolani na Buhongwa juu ya uvumi wa taarifa potofu zilizoenezwa kwenye maeneo hayo zikieleza juu ya mtu aitwaye Teleza na anayedaiwa kubaka, kuwalawiti wanawake na kuwajeruhi.
“Aidha, Jeshi la Polisi linalaani kitendo cha baadhi ya wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kutaka kumshambulia mwananchi eneo la Mtaa wa Ibanda, katika nyumba ya kulala wageni, Kata ya Mkolani, Wilaya ya Nyamagana, saa 4.00 usiku ambaye tulifanikiwa kuokoa maisha yake ambapo walimtuhumu kuwa ni teleza na wakidai kwamba ndiye anaye wabaka na kulawiti wanawake wa maeneo hayo,”imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi hilo limeongeza kuwa; “Taarifa hizo sio za kweli bali ni za kufikirika na kutokana na kitendo hicho, Jeshi la Polisi hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuhusika kutenda uhalifu huo ikiwemo wanaochapisha na kutoa taarifa potofu kwa wananchi, kwani zinaweza kuleta taharuki na uvunjifu wa amani.”