CAF yaongeza mkwanja CHAN | Mwanaspoti

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeweka wazi ongezeko kubwa la zawadi kwa washindi wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) ya mwaka 2024 yatakayofanyika Kenya, Tanzania, na Uganda.

Zawadi ya mshindi wa michuano hii imeongezwa kwa asilimia 75, ambapo sasa mshindi atapata dola 3.5milioni ambazo ni zaidi ya 8.7 bilioni.

Aidha, jumla ya zawadi kwa mashindano haya imeongezwa kwa asilimia 32, na kufikia dola 10.4 milioni ambazo ni zaidi ya 25.8 bilioni.

Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, alisema: “CHAN ni mashindano muhimu kwa maendeleo na ukuaji wa wachezaji wa soka wa Afrika, hasa wale walioko kwenye ligi za ndani, na itachangia pakubwa katika kuongeza ushindani wa kimataifa wa soka la Afrika na mashindano ya CAF.”

Aliongeza kwa kusema, “Mashindano haya ni sehemu ya mikakati yetu ya kuwekeza katika soka la Afrika na kuyafanya kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka, watazamaji wa televisheni, wadhamini, washirika, na wadau wengine, si tu barani Afrika, bali duniani kote.”

Mashindano ya CHAN 2024 yatakayoanza rasmi Februari 1, 2025, na kumalizika Februari 28, 2025, yatashirikisha nchi 17 ambazo tayari zimejihakikishia kufuzu, ikiwa ni pamoja na wenyeji Kenya, Tanzania, na Uganda, pamoja na mataifa mengine makubwa kama vile Morocco, Guinea, Senegal, Mauritania, Niger, Burkina Faso, Nigeria, na mengineyo.

Hii ni habari nzuri kwa soka la Afrika, kwani ongezeko la zawadi linazidi kuvutia timu na wachezaji zaidi, huku ikiongeza hamasa kwa mashabiki wa mchezo huu barani Afrika na duniani kwa ujumla. 

Related Posts