Moto wateketeza makazi ya mastaa Hollywood Marekani

Marekani. Moto wa porini umelipuka eneo la Hollywood Hills na kusababisha taharuki kubwa na watu wengi kuhamishwa kutoka Hollywood Boulevard, huku kukiwa na onyo kwamba wakazi wengine 100,000 wanapaswa kuwa tayari kuondoka makwao.

Kwa mujibu wa tovuti ya daily mail, moto huu wa kasi, unaojulikana kama “Sunset Fire,” ulianza kuenea kwa kasi kupitia Hills, na kusababisha amri ya dharura ya kuhama saa 12 jioni kwa saa za eneo hilo Jumatano, tayari ukiathiri ekari 20 za ardhi karibu na Runyon Canyon.

Watu wasiopungua watano wamepoteza maisha katika janga hilo, huku takriban majengo 1,000 yakiharibiwa kabisa na maelfu ya watu wakibaki bila chochote ila majivu jijini Los Angeles.

Sasa moto umleta madhara makubwa katika kitovu cha mastaa wa filamu nchini humo, ukisababisha eneo maarufu, linalojumuisha Hollywood Walk of Fame, TLC Chinese Theatre, na Hollywood Bowl, kufungwa na watu kuhamishwa.

Tangazo la tahadhari lilisomeka: “Amri ya Lazima ya Kuhama sasa ipo kwa Laurel Canyon Blvd (Magharibi) hadi Mulholland Dr (Kaskazini), 101 Freeway (Mashariki) hadi Hollywood Blvd (Kusini).”

Mashuhuda walioripoti moto huo walisema kwamba moto uliongezeka kwa kasi, kwa sababu eneo hilo lina msitu mnene unaochochea moto kuendelea kusambaa kwa kasi.

Nyota wa Hollywood Ambao Nyumba Zao Zimeungua ni pamoja na John Goodman ambaye nyumba yake iliyoko Pacific Palisades ilikuwa moja kwa moja kwenye njia ya moto huo wa hatari, ambao tayari umeunguza zaidi ya ekari 15,000 na kusonga kwa kasi ya uwanja wa mpira wa miguu tano kwa dakika.

Kitu pekee kilichosalia ni bwawa la kuogelea la nyuma ya nyumba, ambalo bado limejaa maji machafu yenye majivu, pamoja na njia ya gari, ambayo sasa inaelekea kwenye vifusi vya nyumba iliyokuwa hapo awali.

Mwingine ni Anthony Hopkins ambaye ni mshindi wa tuzo ya Oscar. Nyumba yake imeteketezwa kabisa, kama inavyoonyeshwa katika picha za kusikitisha kutoka eneo la tukio.

Malango ambayo yalilinda eneo hilo bado yamesimama, lakini sasa yamefunguka kabisa.

Miti iliyokuwa ikitoa faragha na urembo kwa eneo hilo imeungua na kubaki vichaka vilivyokauka hadi majivu.

Mwingine ni Miles na mkewe Keleigh Teller waliowahi kuigiza filamu ya Top Gun: Maverick.

Wanandoa hayo walinunua nyumba yao kwa $7.5 milioni (Sh18.6 bilioni) Aprili 2023. Sasa, nyumba hiyo imeteketea kabisa kwa moto huo wa porini.

Picha za kushtusha zinaonyesha gari lililokuwa limeegeshwa kwenye njia ya gari mbele ya nyumba hiyo pia limeungua kabisa na kubaki mabaki yaliyoteketea.

Keleigh Teller alituma picha kadhaa za moto huo kupitia Instagram usiku wa tukio. Picha ya kwanza ilionyesha moto ukiwaka kwa nguvu, akiwa ameambatanisha emoji ya kulia, huku picha ya pili ikihimiza watu waliohamishwa kuweka bakuli za maji mitaani kwa ajili ya wanyama waliokuwa wakitoroka moto.

Mwingine ni nyota wa fiilamu ya American Pie, Eugene Levy, ambaye pia amepoteza nyumba yake baada ya moto wa porini kuangamiza mali yake kabisa.

Mapema, Levy alielezea hali ya kukimbia moto huku akikwama kwenye msongamano mkubwa wa magari pamoja na maelfu ya wakazi wengine waliokuwa wakijaribu kuhama kufuatia maagizo ya dharura ya kuhama.

“Moshi ulionekana mweusi sana na mkali juu ya Temescal Canyon. Sikuweza kuona miali ya moto, lakini moshi ulikuwa mzito sana.”

Mwanawe, Dan Levy alitoa kauli ya huzuni kupitia mitandao ya kijamii, akisema:

“Nimevunjika moyo kwa ajili ya familia yangu, marafiki zangu, na watu wa LA waliothiriwa na moto huu mkubwa wa kihistoria.”

Kufikia Jumatano alasiri, maafisa hawakuwa wametoa makadirio kamili ya majengo yaliyoharibiwa au kuharibiwa kabisa na moto huu wa porini.

Hata hivyo, takriban wakazi 100,000 walikuwa chini ya amri ya kuhama, huku karibu majengo 30,000 yakiwa bado yako katika hatari kubwa.

Aidha, watu wengine 100,000 wameonywa kuwa wanapaswa kufikiria kuhama ikiwa hali itazidi kuwa mbaya.

Related Posts