Los Angeles. Moto ulioibuka na kusambaa kwa kasi katika makazi ya watu jijini Los Angeles na katika milima ya Hollywood nchini Marekani, umesababisha vifo vya watu watano huku ukiteketeza majengo ya makazi zaidi ya 1,500.
Tovuti ya The Guardian, imeripoti leo Alhamisi Januari 9, 2025 kuwa moto huo maarufu kama ‘wildfire’ umeibukia katika maeneo sita tofauti jambo ambalo linasababisha ugumu kwa maofisa wa zimamoto nchini humo kukabiliana nao.
Miongoni mwa maeneo ambayo moto huo umeibukia ni pamoja na California ambapo Idara ya Misitu na Kupambana na Moto (Cal Fire) imesema kuna moto ulioibuka ghafla eneo la milima ya Hollywood.
Kwa mujibu wa Cal Fire, tayari moto huo ulioibuka umeshateketeza zaidi ya ekari 10 tangu kuibuka kwake saa 11:57 asubuhi ya leo.
Inaelezwa kwamba upepo ulikuwa umeanza kupungua eneo la Los Angeles, jambo lililosababisha maofisa hao kuanza kuudhibiti kabla ya hali kubadilika ghafla na kusababisha usambae maeneo mengine ikiwemo eneo la Santa Monica.
Zaidi ya wakazi 130,000 wanaoishi katika makazi hayo zaidi ya 1,500 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kuelekea eneo la Pwani ya Bahari ya Pasific kando ya eneo la Pasadena.
“Bado tuko kwenye hatari ya moto huu,” amesema Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto jijini Los Angeles, Kristin M Crowley.
‘Wananchi wanapitia wakati mbaya na wa kutisha hususan ni usiku,” ameeleza.
Janga hilo lilianza Jumanne alasiri, baada ya kimbunga cha upepo kilipoibua vimulimuli vilivyoshika nyasi kisha kuibua moto mkubwa ulioanza kuteketeza maeneo ya misitu na makazi ya watu.
Hadi kufikia asubuhi ya leo, maofisa wa zimamoto walikuwa wamesambazwa maeneo mbalimbali ya California kuzuia moto huo kusambaa na maeneo mengibe ya Mji wa Oregon ili kuudhibiti.
Zimamoto pia imesema maofisa kadhaa wa kikosi hicho wamejeruhiwa wakati wa kupambana na moto huo huku ikidokeza kuwa zaidi ya maofisa 20 wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Wakati moto huo ukiendelea kusambaa, shule zote jijini Los Angeles zimetangaza kufungwa kuanzia leo Alhamisi Januari 9, 2025, ili kuepusha madhara ya janga hilo kwa wanafunzi.
Uamuzi wa kufungwa shule hizo umetangazwa na Mrakibu wa Kikosi cha Zimamoto jijini humo, Alberto Carvalho
Kuhusu wanafunzi wanaokaa bweni, ofisa huyo amesema vinaandaliwa vituo nane vitakavyotumika kama makazi ya dharura kwa ajili ya wanafunzi wote jijini humo ambapo watapatiwa mahitaji ya msingi ikiwemo chakula na malazi.
Mkuu wa Zimamoto jijini Los Angeles, Anthony Marrone, alisema Jumatano kuwa kulikuwa na maofisa wa kutosha kukabiliana na moto katika maeneo manne tofauti, hata hivyo kuibuka kwa moto maeneo mengine kunaweza kuongeza ugumu wa kuudhibiti.
“Kwa upana wa jeshi letu tumejipanga kuweza kupambana na moto unaolipuka porini kwa angalau maeneo mawili tofauti, hata hivyo kuwa na moto maeneo manne tofauti inaweza kutupatia ugumu kupambana nao,” alisema.
Moto ya maeneo ulipopita moto huo umesababisha hasara ya mali inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 50 jambo linaloweza kusababisha mtikisiko wa kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.
Moto huo pia unaathiri vyanzo vya maji nchini humo. Maofisa wamekuwa wakipambana kusukuma maji kwa wingi ili kukabiliana nao bila mafanikio huku mamlaka zikiwataka wananchi kuhifadhi maji ya kutosha.
Mkazi wa eneo la Pacific Palisades, Sheriece Wallace amesema hakuna anafahamu iwapo moto huo ungefika yalipo makazi yake hadi pale dada yake alipopiga simu kuita Helkopta ya kuwaokoa.
“Nilianza kuona kama kunanyesha kumbe Helkopta ilikuwa imeshafika kutuokoa muda mfupi baada ya nyumba yetu kushika moto,” amesema.
Inakadiriwa katika eneo la Palisades pekee, watu takriban 37,000 wameyakimbia makazi yao baada ya moto huo kuunguza sehemu makubwa ya eneo hilo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa Msaada wa Mashirika.