Dk Biteko acharuka Tanesco, aagiza uongozi ufumuliwe

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amekerwa na utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akitoa maagizo uongozi wa kituo cha miito ya simu (call centre) ufumuliwe.

Maagizo ya Dk Biteko kwa Tenesco ni kufuatia kutotekelezwa kwa maagizo yake ya aliyoyatoa mwaka jana ya kuwepo kwa namba ya mawasiliano ya wateja isiyolipiwa agizo ambalo halijatekelezwa.

Dk Biteko ameyatoa maagizo hayo leo Alhamisi Januari 9, 2025 baada ya kutembelea kituo cha miito ya simu Tanesco ambapo amesema watendaji wa shirika hilo wamezoea kazi.

“Mwaka jana baada ya kuja hapa niliona mabadiliko, hawa watu ni kama pendulum tuliyofundishwa kwenye fizikia, mmezoea kazi mmeanza kulala, mmezoea matatizo. Sasa mimi siwezi kukubali kuzoea matatizo bada ya muda mnasema simu ya miito haipo hewani haiwezekani.

“Mnajua uzuri wa huduma inaanza kwa mpokea huduma, ukienda hotelini mapokezi ya pale ndio yanaonyesha kule kuna huduma gani. Mtu akienda Tanesco anajua seriousness (umakini) yenu kwa simu anazopiga hapa, sasa siwezi kukubali tafuteni uongozi mpya hapa, kwa wiki moja nataka hapa pasukwe upya,” amesema.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Miito ya Simu Tanesco, Irene Gowele akijibu swali la Dk Biteko sababu ya kitengo hicho kutotekeleza maagizo yake, amesema tayari namba wameipata. Sababu ya kutokuanza kufanya kazi kwa namba hiyo alimuomba Naibu Waziri Mkuu kumpelekea sababu hizo jambo ambalo lilifuatiwa na tamko la Dk Biteko kutaka uongozi kufumuliwa.

Aprili 4, 2024, Dk Biteko alitembelea kituo hicho na kutoa maelekezo kwa Kituo cha Huduma kwa Tanesco, kuangalia namna ya kuwawezesha wateja kupiga simu bila kulipia gharama.

Dk Biteko amesema Watanzania wengi licha ya kulipia Luku kila mwezi, bado ni maskini na wanatakiwa kuendelea kuhudumiwa na Serikali.

“Lazima muangalie utaratibu wa wateja wetu wanaopiga simu kulipa hela, mimi siamini kwa nini tuendelee kumtoza mteja wetu anayelipia Luku kila mwezi, lakini likitokea tukio moja tunamtoza hela lazima tutafute mazingira ya mteja kupiga simu ahudumiwe bila gharama yoyote,” amesema.

Related Posts