KUNA wash’kaji hapa mtaani wamekuwa wakilalamika sana mara kwa mara pale timu ya taifa inapoitwa wakidai kunatakiwa kuwe na usawa kwa wachezaji kutoka klabu zote.
Kwamba wanataka kuona suala la kuita wachezaji wengi kutoka timu za Simba na Yanga lisipewe kipaumbele na fursa sasa ianze kutolewa kwa wachezaji wengi kutoka timu nyingine.
Wanadai hizo timu nyingine zina wachezaji bora na wanaopata nafasi ya kutosha ya kucheza kuliko hata hao wa Simba na Yanga ambao wamekuwa wakiitwa katika vikosi vya timu za taifa.
Lakini kuna wachache ambao walikuwa wanatetea uteuzi wa wachezaji wa timu za taifa na wenyewe wanaona sawa tu fursa kubwa kutolewa kwa wachezaji wa Yanga, Azam au Simba.
Lilikuwa suala la muda tu na kupitia mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2025 yanayoendelea huko Pemba, Zanzibar kijiweni tumepata majibu kuwa kilichokuwa kinafanyika kuita wachezaji wengi kutoka Azam, Yanga na Simba ni jambo sahihi kuliko wazo la kuwajaza wachezaji wa klabu nyingine.
Katika Kombe la Mapinduzi wengi hao wa timu nyingine wameshindwa kutuonyesha kwa nini tusiwategemee wachezaji wa klabu kubwa katika timu yetu ya taifa kutokana na viwango vya chini ambavyo wengi wamekuwa navyo kwenye hayo mashindano.
Tulitegemea kwa vile wachezaji wa Simba, Yanga na baadhi wa Azam hawapo kikosini, hao wa timu nyingine wangetumia fursa hiyo kuwasuta wale ambao wanaona sawa tu kwa mastaa wetu wa timu kubwa kupewa nafasi kubwa kwenye timu za taifa.
Kuna uzoefu fulani mkubwa na huduma nyingi stahiki ambazo wachezaji wa klabu zetu kubwa wanazipata ambazo zinawafanya wawe na uwezekano mkubwa wa kuziasaidia timu zetu za taifa hata kama hawapati nafasi ya kucheza kulinganisha na wale wa timu nyingine.
Mwisho wa siku mpira ni mchezo wa wazi na leo rasmi umetupatia majibu.