Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana amesema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, zinakusudia kuingiza kwenye mitalaa ya elimu masuala ya haki za binadamu.
Amesema licha ya kuendesha elimu na mafunzo kuhusu haki za binadamu, wanawasiliana kwa karibu na wizara hiyo ili kuona uwezekano wa kuwa somo kufundishwa shuleni.
Dk Chana ameyasema hayo leo Jumapili, Mei 12, 2024 wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, kwa lengo la kujadili kwa pamoja masuala yanayogusa haki za binadamu.
Amesema Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za kitaifa za kulinda haki za binadamu, ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, lakini pia wanaendelea kupitisha sheria zinazolinda haki za binadamu na kufanya marekebisho mbalimbali pale inapohitajika.
“Masuala ya elimu ya haki za binadamu lazima iwe sehemu ya mitalaa yetu, ili mtoto anapofanyiwa ukatili asione hii ndio mila na desturi ya Mtanzania, mtoto ajue kujilinda, kujitetea, kutoa taarifa iwe ni kwa wazazi au kwenye dawati la jinsia ambayo tumejiwekea,” amesema.
Balozi Chana amewataka wadau wa haki za binadamu kufanya kazi kwa ushirikiano ili kama kuna maoni, ushauri, mapendekezo waweze kuwasiliana kwa pamoja ili pale inapohitajika kurekebisha sheria, kuweka mfumo ili Watanzania wote waendelee kuwa na amani.
Aidha, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
“Katika kutimiza azma hiyo Serikali imeendelea kuboresha utoaji haki, kuwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kuwa na Tume ya Haki Jinai,” amesema Chana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema kwenye ripoti yao waliyoizindua April mwaka huu, hali ya haki za binadamu hapa nchini imedorora kwa mwaka 2023 ukilinganisha na mwaka 2022.
Ameyataja makundi yaliyoathirika zaidi ni kundi la watoto kwa asilimia 45, wanawake asilimia 30, watu wenye ulemavu asilimia 10, wazee asilimia 12 na wanaume asilimia 10.
“Kundi linaloathirika zaidi ni la watoto linalosahaulika, wanafanyiwa ukatili mkubwa wa kingono, ubakaji, ulawiti na watoto wa kiume ndio wameathirika zaidi kwa asilimia 80 na ulawiti. Na asilimia 85 wanalawitiwa wakiwa nyumbani na ndugu wa karibu na sisi kama watu wa haki za binadamu lazima tutalifanyia kazi suala hilo,” amesema Dk Anna.