MECHI za hatua ya makundi za mashindano ya klabu Afrika zinahitaji kuzicheza kwa akili na hesabu kubwa kwa sababu zimekaa kimtego sana hivyo zinatakiwa kuendewa kwa adabu.
Na kwa tathmini tuliyoifanya hapa kijiweni, mechi za raundi ya tatu na ya nne za hatua ya makundi ndizo za muhimu kupitiliza na ndio zinatoa uamuzi wa hatima ya timu nyingi kwenye makundi.
Yaani vyovyote utakavyofanya, hakikisha unapata pointi tatu au zaidi katika mechi za raundi ya tatu na ya nne na hilo likishindikana basi utafuzu kwa tabu kwenda raundi inayofuata au pengine utashindwa kabisa kusonga mbele.
Mechi za raundi hiyo ni muhimu kwa sababu timu mbili zinakutana zenyewe kwa zenyewe katika mechi mbili mfululizo hivyo kama angalau unapata pointi tatu, nne au sita, maana yake unakuwa umeshafanikiwa kuvuruga hesabu na mipango ya mpinzani huyo uliyekutana naye.
Na upande mwingine timu mbiki kwenye kundi hilohilo zinakuwa zinakutana hivyo kunakuwa na uwezekano wa timu moja kuangusha pointi na wewe ukafanikiwa kusogea juu au kupunguza pengo la pointi ikiwa utakusanya kwa upande wako.
Ndivyo ambavyo Simba na Yanga zimefanya katika mechi hizo za raundi ya tatu na ya nne kwenye makundi yao ambapo kila moja imevuna kiasi kikubwa cha pointi ambacho kimezifanya ziwe katika nafasi nzuri ya kusonga.
Simba iliyokuwa na pointi tatu na nafasi ya tatu kwenye kundi lake, ikachukua pointi sita dhidi ya CS Sfaxien na kusogea hadi nafasi ya pili katika kundi lake ikipishana kwa tofauti ya mabao tu na kinara CS Constantine ambayo yenyewe iligawana pointi tatu tatu na Onze Bravos ya Angola.
Yanga yenyewe ikavuna pointi nne kwa TP Mazembe ambazo ziliisogeza hadi nafasi ya tatu huku ikipitwa kwa pointi moja tu na MC Alger ambayo iliangusha pointi tano dhidi ya Al Hilal.
Matokeo hayo sasa yameziweka Simba na Yanga katika hitajio la kushinda tu mechi zao ili zitinge robo fainali jambo ambalo halina presha kubwa kulinganisha na iwapo zingehitajika kushinda mechi zao huku zikitegemea matokeo ya wengine. Hesabu tu mwanangu.