Raia Wa Pakistan Nane Kizimbani Kwa Zaidi Ya Kilo 400 za Dawa Za Kulevya

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

RAIA nane wa Pakistan wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kusafirisha zaidi ya kilo 400 za dawa za kulevya.

Katika  hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Titus Aron imewataja washtakiwa hao kuwa ni Mohamed Habifu (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pettilwam (50),Immambakish Kudhabakish (55), Chand Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzal Hussein (45)

Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki kuwa, Novemba 25, 2024 huko katika eneo la Navy Kigamboni jijini Dar es salaam washtakiwa wote walikutwa wakisafirisha  kilo 22.53 za dawa za kulevya aina ya heroine na kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.

Hata hivyo washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao hawakuruhusiwa kujibu kitu chohote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa Mahakama Kuu ama kwa kupewa kibali kutoka kwa DPP

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upepelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Januari 22, 2024 kwa ajali ya kuja kutajwa. Washtakiwa wote wamerudishwa rumande.

 

Related Posts