Ntobi avuliwa uenyekiti Chadema, mwenyewe atoa msimamo

Shinyanga. Kikao cha kamati tendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga jana Jumatano Januari 8, 2025 kimefikia uamuzi wa kumvua uongozi Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 9, 2025 na Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, imesema Ntobi amevuliwa nafasi hiyo kutokana na kukiuka maadili na utovu wa nidhamu ikiwemo kuchafua viongozi wa chama chake kitaifa kupitia mitandao ya kijamii.                                                                             Hata hivyo, kutokana na hatua ya kuvuliwa nafasi hiyo Ntobi amedai kuonewa kwa maamuzi hayo huku akisema kuwa atakata rufaa kupingana na maamuzi hayo.

“Ni kweli nimevuliwa uongozi lakini nimeonewa kwa sababu nilitakiwa kufikishwa kwenye dawati la nidhamu ili nisikilizwe kwa upande wangu lakini kamati ilikaa na kufanya uamuzi bila kunifikisha kwenye dawati la nidhamu na kwa sasa wakili wangu anashughulikia suala la kukata rufaa” amesema Ntobi.

Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amekanusha madai ya Ntobi ya kutosikilizwa kwa sababu kabla ya kufanya uamuzi, husikiliza upande wa pili Ili kujitetea na Ntobi alipewa nafasi hiyo.

Related Posts