Wiki moja ya kwanza ya mwaka 2025 imekatika na sasa tunasubiriwa na wiki 51 kuzifanyia kazi ikiwamo ile muhimu ya uchaguzi mkuu wa nchi.
Wastaafu watakuwa na kazi kubwa ya kumjua na kumpigia kura yule wanayeamini ataweza kuzifanyia kazi hali zao duni, hasa atakayewaongezea pensheni yao ifike japo Sh300,000 kwa mwezi.
Inawezekana, hasa kama Siri-kali itakayochaguliwa kuingia madarakani itakapolichukua na kulifanyia kazi kweli hili wanalosema kwa mdomo tu, la kuwawezesha wastaafu wa Taifa hili kuwa na hali njema ya maisha na kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha ili kila mtu awe mwajiriwa, mstaafu au mwana kikokotoo mtarajiwa, ingawa hali ngumu ya maisha inambana zaidi mstaafu tu!
Mstaafu wetu anategemea kuwa Siri-kali itakayochaguliwa kuingia madarakani kama kweli itataka wastaafu wa Taifa hili wawe na hali nzuri ya maisha, ianze kwa kuyafanyia kazi mara moja mambo matatu makubwa, ambayo ni kupandisha pensheni kuwa Sh300,000 kwa mwezi, kurudisha matibabu ya bure kwa wazee wenye miaka 60 na zaidi na kuwaanzishia wastaafu benki ya wastaafu itakayowapa mikopo yenye riba nafuu. Yapo mengi yanayowasibu wastaafu lakini tuanzie hapo.
Inafikirisha sana pale mstaafu wa Taifa anapotegemewa kuwa na hali nzuri ya maisha kwa pensheni ya Sh150,000 kwa mwezi, tofauti kubwa na mwakilishi wake kule ‘Domdom’ ambaye anatia ndani shilingi milioni… mama wee… 14 ambazo pamoja na marupurupu na marapurapu yake mshahara unafika Sh16 milioni kwa mwezi, rudia hapo, kwa mwezi, kwenye nchi hii hii moja tunayoaminishwa na kibwagizo cha ‘binadamu wote ni sawa.’
Wastaafu na waajiriwa ambao ni wastaafu watarajiwa wanadhani kuwa huu mshahara wa wawakilishi wao bungeni unafaa kukatwa panga na kupunguzwa kuwa Sh10 milionikwa mwezi, hata milioni tano kwa mwezi, kubana matumizi ili zinazopatikana wastaafu wa Taifa waweze kuongezwa pensheni yao.
Nchi hii si ni yetu wote? Kwa nini wengine waishi peponi na wengine waishi Jehanamu, hapahapa duniani? Mwakilishi atakayeuona mshahara huo ni mdogo aachie ngazi mchuma upuyange!
Mstaafu wetu anakwenda mbele kidogo, anafikiria pale nje kidogo ya ‘Domdom’ kuanzishwe shamba kubwa ambalo ile miezi yenye mvua waheshimiwa wawakilishi watatakiwa kupiga jembe kuzalisha chakula ili waone tabu wanazopata wakulima.
Kwa mpango huu wataweza kuwakumbuka wastaafu wakulima na wataweza kuwafanyia utaratibu wa kurudisha tena matibabu ya bure kwa wazee wenye miaka 60 na zaidi ili nao wamung’unye keki ya Taifa letu.
Siyo shamba tu ‘Domdom,’ utaratibu maalumu unaweza kufanywa ili Mtwara wakivuna korosho baadhi ya waheshimiwa wanakwenda huko, Kagera wakivuna ndizi waheshimiwa wanakuwa huko kusaidia kuvuna, halikadhalika Kilimanjazo wakivuna kahawa waheshimiwa wako huko, Tabora wakivuna tumbaku wawakilishi wengine wanakwenda huko na Mbeya wanapovuna mpunga waheshimiwa wako huko wakiwapa tafu wakulima.
Mstaafu wetu anapenda kuamini kwamba, hakuna mheshimiwa atakayeingia mitini kuwawakilisha wakulima kwa kanuni hii.
Ni wazi kuwa, waheshimiwa wetu watakuwa imara zaidi kuliko wakicheza mpira ili kutoka jasho na wawakilishi wenzao wa nchi jirani.
Ni wazi kuwa, wawakilishi wetu wataielewa hali halisi ya tabu wanazokumbana nazo wakulima wetu wakati wa kulima na kuvuna ili kuilisha nchi.
Kwa kawaida hii ya kuingia shambani mara moja kwa mwaka mstaafu wetu anaamini wawakilishi watafanya haraka kuwatafutia wakulima wetu cha kujipoza nacho, wakianza na ‘matibabu ya bure kwa wazee.’
Naam, wiki moja ya mwanzo ya mwaka mpya 2025 imeishakatika na tumebaki na wiki 51.
Tunaweza kusameheana hizi wiki mbili zilizobaki ili kuumaliza mwezi huu wa ‘Njaanuari.’
Tunaweza kukubaliana kusameheana maana watu wako bize na kulipa kodi, kulipa ada za watoto wao na kununua sare za shule wanazosoma huku babu na bibi zao wakisubiri nyongeza ya pensheni yao ambayo bado ‘ina jambo letu’ kwenye makaratasi, badala ya kuwa mifukoni mwa wastaafu.
Tukiishamalizana na ‘Njaanuari’ na tabu zake, wote tushikane mikono kweli ili kuibadili Tanzania yetu iwe Tanzania kweli. Hili la kutaka wastaafu wetu kuwa na hali njema ya maisha yao lifanyiwe kazi kweli-kweli na lisiishie kuwa maneno ya kanga tu kama yalivyoishia yale ya matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi. Inawezekana, ni utashi tu unatakiwa kwa waheshimiwa wetu.
Nchi hii ni yetu sote na aliyeliunda Taifa na kuijenga nchi ni mstaafu wa kima cha chini, kama siyo cha chizi ambaye mpaka leo bado anapokea ‘Laki si pesa’ ya laki moja kamili wakati hiyo hamsini anayoambiwa ameongezwa bado iko kwenye makaratasi ikisubiri ‘jambo letu’, badala ya kuwa mifukoni mwa wastaafu.
Wastaafu tusije tukaishia kujifariji kwa alivyoimba mjukuu wetu mmoja maneno yanayofikirisha: “Bora ni enjoy, maisha mafupi ni simple. Ya nini niteseke roho, jiunge nami upoze koo.”
Mwaka 2025 umebisha hodi. Maisha ya mstaafu wetu ni mafupi. Tujitahidi kuyafanya simple. Tujiunge naye tumpoze koo… kwa maji ya bombani na siyo yale ya Ilala!