Mwongozo kwa wanaojitolea waja | Mwananchi

Dodoma. Serikali ya Tanzania inakamilisha mwongozo kwa vijana wanaojitolea utakaiwawezesha kupatiwa malipo wakati wa utumishi wao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe.

Katika swali la nyongeza, Sichalwe amesema kuna vijana wengi wanaojitolea ambao wengine wamefanya hivyo hadi miaka mitano.

Amesema kitendo hicho kinavunja moyo sana vijana wakitanzania kujitolea.

“Je wizara inaonaje kuziandikia waraka halmashauri nchini angalau kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana hawa kwasababu nao ni binadamu na wanamaisha yao na familia zao,”amesema Sichalwe.

Akijibu swali hilo, Simbachawene amesema suala hilo la kujitolea linahitaji kufikiriwa sana.

“Nakumbuka kuwa Bunge hili lilituagiza tutengeneza mwongozo wa vijana wetu waliohitimu ambao wanajitolea katika maeneo mbalimbali. Na tunapoandaa mwongozo huu tumekutana na vitu vya kimgongano sana,”amesema.

Ametoa mfano wa vitu vya kimgongano walivyokutana navyo ni wanawaweka vipi wale wanaojitolea serikalini na wale kwenye sekta binafsi.

Simbachawene amesema jambo hilo limewapa kazi kubwa ya kufikiria.

“Sasa tumeshajiandaa na tunahitimisha tunapeleka Bakita (Baraza la Kiswahili la Taifa) wanatafsiri ile lugha baadaye tutatoa huu mwongozo na kila mmoja aliona,”amesema Simbachawene.

Amesema miongoni ni namna gani wafanyakazi wanaojitolea watakuwa wanapata angalau malipo yanayoeleweka na kutakuwa na formula (utaratibu) unaoeleweka.

Katika swali la msingi, Mbunge wa viti maalumu Shally Raymond ametaka kufahamu ni vijana wangapi wa vyuo wanafanya kazi ya kujitolea na wangapi wameajiriwa na kujiajiri baada ya kujitolea.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi amesema Serikali ilianza rasmi kuratibu utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa Wahitimu (internship) mwaka 2019/20.

“Tangu kuanza utekelezaji wa programu hii, jumla ya wahitimu 21,280 wamenufaika, wanaume ni 11,281 na wanawake ni 9,999,”amesema.

Amesema miongoni mwa wanufaika hao, jumla ya wahitimu 3,772 wamepata kazi, wanaume wakiwa ni 2,265 na wanawake 1,507.

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *